
Mmoja wa wanamuziki waliowahi kutesa sana na kutengeneza hela kwa hali ya juu Bongo Lucas Mkenda a.k.a Mr Nice ameibuka na kujibu tuhuma za kuambiwa kuwa amefilisika
“Mimi sijafulia bado niko juu kisanaa na muziki wangu haujachuja hata siku moja, hivyo watu wanaodai nimefulia pengine hawafahamu mipango yangu,” alianza kwa kujitetea alipokuwa anazungumza na Dar41.
“Hili suala la kufulia,limetoka wapi na nini maana ya mtu kufulia sioni sababu ya watu kusema nimefulia, sijafulia hao wanaosema hivyo wanasababu zao.”
“Huwezi kusema kuwa nimefulia kimuziki ama kifedha wakati aina ya muziki wangu hakuna mtu anaweza kuiga wala kuifanya bado niko mwenyewe na matoleo niliyoyatoa bado yanafanya vizuri sokoni.
“Kama kukaa kimya bila kutoa albamu mpya au kupanda jukwaani ama kutonyesha uwezo wako kifedha ndiyo maana ya kufulia basi mimi sijafulia tena niko juu zaidi.”
“Kuna watu waliofulia tunawafahamu na hatuwezi kuwasema walianza muziki kwa mbwembwe na baadaye wakakwama ghafla na hii ilitokana na kubebwa bebwa tu na baadhi ya watu kwa sababu ya faida za wachache lakini sio kweli kwamba wanauwezo mkubwa kisanaa.
“Baada ya kutoa visingo vyao ama albam zao za kuunga unga wakajiona masikio yanazidi kichwa na walipo achwa ili waonyeshe uwezo wao wenyewe wakashindwa hao ndiyo waliofulia sio mimi bwana mi niko juu sana.
“Ingawa kila msanii ana mipango yake kuhusu muziki ila mimi mipango yangu ni ya kimataifa zaidi na kamwe mtu hawezi kufahamu ninachofikiria katika suala zima la muziki ndiyo maana baadhi ya watu wanajaribu kutafuta maneno ya kusema juu yangu lakini ukweli ni kwamba mimi ni zaidi ya wanavyofikiria.”
“Ingawa ni vigumu kukataza watu wasiseme yale wanachofikiria lakini masuala mengine yanakera kuona mtu anasema mambo asiyokuwa na uhakika nayo. Kuthibitisha ninayoyasema nimepanua kazi yangu zaidi katika majukwaa ya kimataifa na hivi karibuni hilo litakuwa wazi.
“Mimi muziki kwangu ni kazi na ndiyo ajira yangu hivyo ni lazima niwe na malengo makubwa ili ninufaike katika maisha yangu yote kwa sababu nimebaini kuwa ni kazi pekee inayonifaa na kunipa mafanikio makubwa ndani na nje ya nchi.