Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Wednesday, June 9, 2010

Mamba aonekana maeneo ya Kinondoni!!


Mnyama pori aina ya mamba anayeishi majini, amepatikana katika bwawa dogo lililoko katika eneo la mpaka kati ya mtaa wa Kumbukumbu Block 41 na ule wa ADA Estate kata ya Kinondoni, suala lililozua wasiwasi kwa baadhi ya wakazi katika eneo hilo.

Kwa nyakati tofauti wakazi wa jirani na eneo la Bwawa hilo, wameeleza kuwa mnyama huyo si wa kwanza na kwamba alishapatikana tena mwingine kaika kipindi cha nyuma na walipotoa taarifa kwa idara za mali asili, mnyama huyo alichukuliwa na kuhamishwa, lakini siku za karibuni ameonekana tena mwingine.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Kumbukumbu Block 41 Majeshi Shabani amethibitisha kuwepo kwa taarifa hizo, na kueleza kuwa mbioni kuliripoti suala hilo kwa watu wa Mali asili ili kumuondoa.

Amesema ni vyema kuchukua tahadhari mapema kabla ya athari, na hasa kwa kuzingatia kuwa ni kinyume na utaratibu na ni hatari kwa wanyama kama hao kuishi katikati ya makazi ya watu ndani ya eneo la jiji.

TAKUKURU waishutumu Polisi kwa Rushwa!!


Maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), wamelishutumu jeshi la Polisi Wilayani Kiteto mkoani Manyara kwa kuwa mstari wa mbele kudai rushwa waziwazi katika mazingira mbalimbali ya kazi zao Wilayani humo.

Katika taarifa yao kwa ujumbe wa mbio za Mwenge unaopita katika Wilaya hiyo, TAKUKURU wameliorodhesha Jeshi la Polisi katika sakata hilo, wakifuatiwa na Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya na Kata,huku wakibainisha jumla ya tuhuma 110 pamoja na malalmiko 102 yaliyoripotiwa dhidi yao.

Naye Mratibu wa Jeshi la Polisi Wilayani Kiteto Morris Okinda amekiri kuwapo kwa changamoto hizo hasa kwa Kikosi cha polisi wa usalama barabarani, na kuihimiza uadilifu ndani jeshi hilo. Ujumbe wa Mwenge wa Uhuru umekuwa na mada ya kupinga rushwa katika jamii.

MwanaCCM azua tafrani msibani!


Katika hali ya kushangaza huku wengi wetu tukiamini hali imeanza kuwa tight miongoni mwa politicians wa hapa bongo hususan kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilayani Mpanda mkoani Rukwa, amesababisha mtafaruku msibani baada ya kutangaza nia yake ya kugombea udiwani katika msiba wa ndugu yake ambaye ni mmoja wa wazee maarufu mjini humo.

Tukio hilo limetokea juzi mchana katika Mtaa wa Mji wa zamani katika Kata ya Kashaulili wakati waombolezaji wa msiba wa marehemu Matwiri Igembesao walipokuwa wanatangaziwa utaratibu wa jinsi ya msiba utakavyoombolezwa.

Ndipo mgombea huyo aliyetambuliwa kama Salumu Mbegele alipokwenda kushika kipaza sauti na kutangaza nia yake ya kugombea udiwani kwa tiketi ya CCM, Kata ya Kashaulili mbele ya Meya wa Mji wa Mpanda, Yasssin Kantampa ambaye pia ni Diwani wa Kashaulili.

Mbegele alisema yeye ni mzaliwa wa Mpanda kwa hiyo anatumia haki yake ya kikatiba kugombea nafasi hiyo ya kisiasa katani humo na alitumia fursa hiyo kuwaomba waombolezaji hususani wanachama wa CCM watakaoshiriki kupiga kura za maoni basi wamchague ili awatumikie katika kutatua matatizo yao ya kijamii ambayo ni kero kwao.

Baada ya Mbegele kutangaza nia yake hiyo, waombolezaji walianza kuondoka msibani hapo kwa hasira huku wakiguna na kudai pale msibani hapakuwa mahali pa kutangazia nia ya kugombea udiwani.

TUCTA acheni kutudanganya, sie watu wazima jamani!!


Vyanzo vya kuaminika vinanyunyiza kwamba eti...shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), linacheza usanii wa kipolitiki baada ya juzi kutoa tamko la kuipa serikali ya JK siku saba kuanzia juzi iwe imepandisha mishahara ya wapigakazi au itaitisha upya mgomo wa nchi nzima.

Wadadisi wanadai kuwa wamegundua mkwara huo ni wa kisiasa kwa ajili ya kuwapiga changa la macho wafanyakazi ili waonekane wana ubavu wakati ukweli unabaki palepale kuwa tayari yapo makubaliano tangu Mei 8, mwaka huu ya kupandisha mishahara.

Kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika, Tucta na Serikali walifikia makubaliano hayo kuwa serikali iongeze mishahara hiyo na hilo litatelezwa katika bajeti ijayo ya serikali itakayosomwa bungeni Dodoma Alhamisi wiki hii.

“Makubaliano yamefanyika kati ya Tucta na Serikali kuhusiana na masuala hayo ya mishahara ya wafanyakazi".

" Kimsingi ni kuwa wamekubaliana kuwa mishahara mipya itatangazwa katika bajeti ijayo ambayo itasomwa Juni kumi…sasa hawa wanacheza mchezo wa usanii wa kisiasa,” kilieleza chanzo chetu na kuongeza: “Wanafanya hivyo kwa sababu wanajua ndani ya siku hizo saba, serikali itasoma bajeti yake na mishahara itapandishwa na serikali, hivyo wanataka watambe kwa wafanyakazi kwamba ‘mmeona serikali imesalimu amri, ipandishe mishahara’ wakati haya ni makubaliano ya tangu Mei nane mwaka huu.

Eti CCJ kuungana na CHADEMA??


Wakati ile sinema ya kuigiza ikiendelea kati ya Chama cha Jamii CCJ na msajili wa vyama vya siasa..kuhusiana na utata wa usajili wa kudumu wa chama hicho.

Mabosi wa chama hicho..kana kwamba wameshaanza kusoma alama za nyakati..kuwa hawana lao kwa uchaguzi wa mwaka...kitendo kilichowafanya waamke gizani hapo jana na kutangazia wafuasi wake waiunge mkono Chadema kama msajili huyo hatawapa kabisa usajili wa kushiriki uchaguzi wa Oktoba.

Kauli hiyo ya kustua ya CCJ kutangazia wafuasi wake kuunga mkono Chadema inakuja kipindi ambacho chama hicho kimetangaza kufungua kesi mahakamani kutaka uhakiki wa wanachama wake usitishwe kwa tuhuma za kukiukwa taratibu.

Naibu Katiba Mkuu wa CCJ Dickson Ng'hily, alitangaza hilo kwa kutaka Watanzania kuunga mkono Chadema kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba kwani lengo la kuanzishwa chama hicho ni kuiondoa CCM madarakani.

Ng'hily ambaye kiongozi ni msaidizi wa mtendaji mkuu wa chama, alitoa kauli hiyo wakati wa matembeza ya amani yaliyoandaliwa na Chadema, maalumu kwa ajili ya kurudisha fomu kwa wanachama wanaotaka kuwania nafasi za ubunge na udiwani kwa jimbo la Ubungo.

“Wakati tunaanzisha CCJ tuliwaambia CCM kuwa watanzania wamechoka na wanataka mabadiliko, kwakuwa lengo kuu la CCJ ni kuleta mabadiliko niwaombe watanzania kuunga mkono Chadema kwani sera zake zimeonyesha dhamira ya kweli ya kufikia huko,”alifafanua Ng'hily

Aliongeza kwamba, kauli mbiu ya Chadema kwamba, ‘‘hakuna kulala hadi kieleweke inaonyesha wazi kuwa wanachama hao na viongozi wao wamejitoa mhanga kwa ajili ya kutetea rasilimali za watanzania.’’

Vibaka wafanya sherehe kwenye gemu la Brazil na Stars!



Watu kutoka mataifa mbalimbali wakiwemo mapaparazi wa kigeni walioambatana na wazee wa samba 'timu ya Brazil', hakika hawatakosa cha kuhadithia wataporudi makwao...baada ya kujikuta wakiingia mitegoni mwa vibaka wa kibongo na kupoteza vitu vyao kadhaa zikiwemo pochi zao zilizokuwa na mikwanja ya kujikimu wakati wakiwa katika kazi yao nje ya Uwanja wa Taifa.

Sinema hiyo ambayo kwasisi watoto wa uswazi mara nyingi tumekuwa tukiistukia na kujiweka sawa,ilitokea muda mfupi kabla ya kuanza kwa mechi hiyo, wakati waandishi hao wakipiga picha nje ya uwanja, wakati huo watu wakiwa katika harakati za kuingia uwanjani kuzishuhudia Taifa Stars na Brazil.

Walichofanya vibaka hao ni kuwahadaa waandishi hao kwa kuwatisha kuwa kwanini wanapiga picha katika eneo hilo, wakati wakijaribu kujieleza, kibaka mmoja aliyekuwa nyuma ya mwandishi mmojawapo, akachomoa pochi na kukimbia.

Licha ya kuwapo askari eneo la nje ya uwanja, vibaka hao walitumia mbinu kali na kufanikiwa kutokomea, licha ya juhudi kubwa za askari polisi.


Tukio jingine ambalo nalo litabaki kama kumbukumbu isiyopendeza, ni kugoma kwa ‘CD’ ya wimbo wa taifa kwa kuimbwa nusu yake, tofauti na ule wa Brazil ambao uliimbwa hadi mwisho.

Hii imedhihirisha jinsi Tanzania ilivyo nyuma, kwani licha ya kuwapo kwa njia nyingi za kiteknolojia, lakini wimbo ya taifa hadi leo bado unahifadhiwa kwenye mfumo wa CD.

Baada ya CD hiyo kugoma, maelfu ya mashabiki waliokuwa uwanjani walishindwa kuvumilia kuonyesha hasira zao wazi, wakaamua kuzomea. Yote haya yanapaswa kuwa funzo kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na serikali kwa ujumla.

Kwa kuwa mechi ya Brazil ni ya kihistoria kwa Tanzania, hata maandalizi yake yalipaswa kuwa ya kiwango cha juu, tofauti na ilivyokuwa.

Iran kuwekewa vikwazo vipya na UN!



Baraza la usalama la umoja wa matiafa limeafikia azimio la kuiwekea Iran vikwazo vipya na linatarajiwa kupigia kura azimio hilo hapo kesho.
Vikwazo hivyo vinalenga kudhibiti miradi ya Nuclear ya Iran, na iwapo vitaidhinishwa basi vitaongeza ukaguzi wa bidhaa zinazoingizwa nchini humo na kupunguza kuuziwa nchi hiyo silaha.

Mwandishi wa BBC katika umoja huo amesema kuwa kuna baadhi ya nchi ambazo hazitarajiwi kupigia kura azimio hilo japo hazina kura ya turufu.

Uturuki na Brazil wamesisitiza kuwa vikwazo vipya kwa Iran vitahujumu uhusiano mwema katika eneo hilo na wamesema kuwa kuna matumaini ya kuendeleza uhusiano wa kidiplomasia kutokana na makubaliano ya kubadilishana mafuta ya nuclear walioafikia hivi majuzi.