Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Thursday, February 25, 2010

WAZIRI MKUU MH.PINDA ATOA TAMKO HANA KIU NA IKULU!


Waziri Mkuu ametoa msimamo huo jana mjini Tabora, baada ya mshairi Ramadhan Katwila ‘ Mv Liemba’, kusoma shairi akimwomba Mungu kumjaalia awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza ngwe yake mwaka 2015.

Pinda amesema hana hamu ya kuwa Rais, kwa sababu ni kazi ngumu tofauti na watu wanavyofikiri.

“Baba wa Taifa (Mwalimu Nyerere) alisema Ikulu si mahali pa kukimbilia, msifikiri kauli ile ni ya uongo.“Urais ni kazi ngumu. Hata hii kazi ya uwaziri mkuu ni ngumu sana, sema kwa vile tu ni lazima mzigo mzito akabidhiwe ‘Mnyamwezi’.

“Ni kazi ambayo kila mtu anakutupia lawama hata ambazo hustahili. Utasikia mwingine anasema kwanza liangalie lilivyo, kila siku utaandamwa na magazeti na kila mara utajikuta kwenye ‘The Komedi’,” alisema Waziri Mkuu.

Hata hivyo, alisema atakuwa tayari kumuunga mkono mtu yeyote atakayejitokeza kuwania urais baada ya kipindi cha Rais Kikwete kumalizika.

Awali Mwenyekiti mstaafu wa CCM wa Mkoa wa Tabora, Juma Nkumba, alimwomba Mungu ampe rehema Rais Kikwete aweze kumteua tena Pinda kuwa Waziri Mkuu mara baada ya kushinda uchaguzi mkuu ujao.

Jana Waziri Mkuu alikagua bwawa na lambo la Imalamihayo ambalo linatumika kama kuogesha mifugo ya wafugaji wa eneo hilo.

Akihutubia wafugaji hao, Pinda aliwataka wapunguze idadi ya mifugo ili kufuga kisasa na kuongeza tija na faida.

Alisema wilaya ya Tabora ina ng’ombe 54,000 ambao ni wengi kulingana na eneo hilo na hivyo kuathiri malisho ya mifugo hao hatua ambayo inawafanya kukosa afya inayotakiwa.

Baadaye Waziri Mkuu alifungua sekondari ya Nkumba ambayo ni kwa ajili ya wakazi wa kata ya Uyui na ambayo inakabiliwa na uchache wa walimu, ukosefu wa maabara, umeme na maji.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Tabora Mjini, Siraju Kaboyonga, aliwachangia wafugaji wa Imalamihayo Sh 100,000 na kutangaza kujenga kisima cha maji shuleni Nkumba, hatua ambayo wananchi katika jimbo hilo walisema angeifanya mapema bila kusubiri ujio wa Waziri Mkuu.
Na mwana habari wetu DSM

No comments:

Post a Comment