Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Wednesday, August 18, 2010

Mtoto wa Kingunge adaiwa kutapeli Sh mil 424

MTOTO wa mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru, Tonny Mwiru amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kisutu, Dar es Salaam, akikabiliwa na mashitaka ya kujipatia Sh milioni 424 kwa njia za udanganyifu.

Inspecta wa polisi, Emma Mkonyi, leo amesoma mashitaka yanayomkabili mtoto huyo wa Mbunge wa Kuteuliwa.

Katika shitaka la kwanza,mshitakiwa Mwiru, kwa kushirikiana na wenzake wasiofahamika, katika tarehe na mahali pasipofahamika jijini Dar es Salaam walikula njama ya kuiibia kampuni ya SCI (TZ) LTD kiasi hicho cha fedha.

Katika shitaka la pili, mshitakiwa alidaiwa kughushi fomu ya benki ya kuhamishia fedha yenye namba E17 ya Agosti 29, 2008.

Kwa mujibu wa Mkonyi, kijana huyo alighushi fomu hiyo kwa nia ya kuonesha kuwa ilikuwa halali na imesainiwa na Ravishankar Rasiman, Mkurugenzi wa kampuni hiyo huku akifahamu si kweli.

Shitaka la tatu, amedaiwa mahakamani kuwa, Agosti 29, 2008, katika benki ya Barclays katika Mtaa wa Ohio, Dar es Salaam aliwasilisha fomu hiyo kwa mfanyakazi wa benki hiyo,Bituni Chiza,huku akifahamu kuwa haikuwa halali.

Imedaiwa pia kuwa,kati ya Septemba na Octoba 2008 katika benki ya CRDB tawi la Kijitonyama, Dar es Salaam mshitakiwa alijipatia Sh 424,458,799.29 kutoka katika akaunti namba 01j014293000 akionyesha kuwa fedha hizo ni halali zimetolewa na kampuni ya SCI (TZ) LMD kwenda kwenye kampuni ya Temm Power Solution.

Mshitakiwa huyo amerudishwa rumande baada ya kukana mashitaka yote na kushindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyomtaka kuwa na wadhamini wawili.

Mwiru pia alitakiwa atoe Sh milioni 10 pamoja na hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.Kesi hiyo itatajwa Agosti 31 mwaka huu.

Hakimu Mkazi, Gabriel Mirumbe, alimuuliza kama Tonny ni mtoto wa Kingunge Ngombale Mwiru,akajibu kuwa Kingunge ni baba yake mzazi.

No comments:

Post a Comment