Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Wednesday, September 29, 2010

Andrew Chenge akamatwe haraka- Mahakama Yatoa Amri
BAADA ya kutoonekana mahakamani jana , Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kinondoni, Dar es Salaam imeamuru kukamatwa kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.
Chenge ambaye yuko nje kwa dhamana akikabiliwa na mashitaka ya kusababisha vifo vya watu wawili, jana hakufika mahakamani hapo wala mdhamini wake bila taarifa.
Amri hiyo ilitolewa mahakamani hapo na Hakimu Sundi Fimbo, baada ya mwendesha mashitaka, Richard Rweyongeza kusoma maelezo ya awali ya mashitaka yanayomkabili mshitakiwa.

“Haijalishi kuwa mshitakiwa yuko kwenye kampeni au wapi, Mahakama haitambui jambo lolote kuhusu kampeni, hivyo kwa kuwa hajahudhuria mahali hapa, inabidi akamatwe kwa kushindwa kutekeleza amri ya Mahakama,” alisema Hakimu Fimbo.
Alifikia uamuzi huo baada ya masharti ya dhamana ambayo yanamtaka mshitakiwa kufika mahakamani siku ya kesi aliyopangiwa na bila hivyo atoe taarifa za kutofika kwake mahakamani.

Kwa niaba ya Hakimu Mkazi, Kwey Rusema, ambaye anasikiliza kesi hiyo, Hakimu Fimbo aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 5 mwaka huu itakaposikilizwa tena.
Ilidaiwa kuwa Machi 27, 2007 mshitakiwa akiendesha gari aina ya Toyota Hilux namba T 512 ACE alimgonga mwendesha pikipiki ya magurudumu matatu - bajaj jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo vya Beatrice Costantine na Victoria George.
Awali baada ya Mahakama kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka, Mahakama ilisema Chenge ana kesi ya kujibu na alitakiwa kufika mahakamani jana kuanza kusikiliza utetezi wake.

Chenge ambaye anatetea ubunge Bariadi Magharibi alisema ataleta mashahidi wawili ambao ni yeye na shahidi mwingine ambaye hakutajwa mahakamani.
Aidha, katika kesi hiyo shahidi wa mwisho wa upande wa mashitaka, Raymond Njeje, alidai kuwa stika ya bima aliyokuwa akitumia Chenge si mali yake.
Njeje alidai kuwa, stika hiyo ni ya gari namba T 571 AKH aina ya Toyota RAV4 nyeusi na si ya Toyota Hilux iliyosajiliwa kwa namba T 513 ACE ambalo alikuwa akiendesha Chenge wakati anapata ajali.

Alidai stika hiyo namba 11919156 inamilikiwa na Evarist Ses iliyotolewa mwaka 2007 kwa ajili ya matumizi ya miezi mitatu kuanzia Juni 29 hadi Septemba 28.

No comments:

Post a Comment