Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Monday, September 27, 2010

Madini yaliingizia Taifa Trilioni 5!!


SEKTA ya madini nchini imeingiza kiasi cha sh trilioni tano, kwa kipindi cha miaka mitano ya utawala wa Awamu ya Nne, lakini kiasi hicho cha fedha hakijaweza kukidhi bajeti ya elimu iliyofikia zaidi ya sh trilioni nane.

Takwimu hizo zilitolewa juzi na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alipokuwa akiwahutubia wananchi waliofika kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za ubunge wa CCM Jimbo la Buchosa, wilayani Sengerema, mkoani Mwanza, zilizofanyika Kata ya Nyakarilo -Buchosa.

Waziri Ngeleja alisema kiasi hicho cha fedha kimetumika kwenye huduma mbalimbali za maendeleo ya taifa na wananchi wake na kamwe si rahisi kwa chama au mgombea kuahidi na kutekeleza ahadi ya kutoa elimu bure.

Alisema pamoja na baadhi ya wagombea kujinasibu kuwa wana uwezo wa kutoa elimu ya bure kwa kutegemea mapato yatokanayo na sekta ya madini jambo hilo haliwezekani kwa sababu kinachopatikana ni kidogo kulinganisha na mahitaji.

“Wananchi msije mkapotoshwa na ahadi hizi za wagombea kutoka upinzani eti watatoa elimu bure kwa fedha za madini…hiyo haiwezekani hata kidogo, mwaka 2005 hadi mwaka huu 2010, sekta ya madini hapa nchini imeingizia serikali sh trilioni tano, zitatoshaje kwenye sekta ya elimu?” alihoji.

Waziri Ngeleja alibainisha kuwa mataifa tajiri duniani yanayoendesha migodi kwa miaka mingi, ikiwamo Marekani, hakuna wawekezaji wanaolipa kodi zaidi ya asilimia 50 ya pato la uzalishaji unaopatikana.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo katika sekta zote hutegemea bajeti ya serikali, hivyo mtu binafsi hawezi kusema atatekeleza ahadi zake bila kupitia mipango ya serikali yenyewe.

No comments:

Post a Comment