Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Tuesday, September 7, 2010

Mrisho Mpoto: Watanzania Tunakufa Kwa Roho Chafu!


JUZI hapa nilipata bahati ya kusafiri na Mrisho Mpoto. Safari yetu ilianzia Iringa kwenda Njombe. Tulikuwa na saa tatu pamoja kujadili masuala juu ya jamii yetu.

Mpoto ni mmoja wa wasanii mahiri na maarufu sana nchini kwa sasa. Na kwangu mimi, Mpoto ni mwanafalsafa anayeifikia jamii pana kwa tungo zake zenye kufikirisha.

Tulipofika eneo la Nyororo, Mufindi, Mpoto alishuka kwenye gari ili tununue chupa ya maji ya kunywa. Ndani ya dakika tatu tukawa tumezungukwa na watu wasiopungua 50. Wote walitaka kumwona Mpoto na kuzungumza naye. Sauti za ’ Mjomba, Mjomba!” zilisikika zikiita.

Tuliondoka mahali hapo baada ya yeye kupiga picha ya pamoja na mashabiki wake. Baadaye alinitamkia; ” Hawa ndio watu wangu, leo wananikubali kwa kuwa nawasemea. Siku nikiacha kuwasemea, watapatwa na huzuni. Watanikataa, nami sitakuwa mtu mwenye furaha pia”. Hapo tukajikita katika kujadili maana ya msanii au mwandishi kuwa kioo cha jamii.

Baadaye kwenye mazungumzo yetu niligusia kauli ya Mpoto kwenye moja ya matangazo ya kijamii redioni. Kwenye tangazo hilo anatamka; ” Kwenda huko, utakufa kwa roho yako mbaya!”.

Nilimwuliza Mpoto swali la kifalsafa; ”Je, binadamu tunakufa kwa roho mbaya au roho chafu?”

”Kaka Maggid, naiona mantiki ya swali lako. Kama nitakunjua viganja vyangu na kuitema roho yangu kisha nikaiangalia… lakini fafanua kwanza fikra zako,” alijibu Mpoto.

Nikafafanua, kuwa binadamu hatukuumbwa kuwa wengine wana roho mbaya na wengine nzuri. Sote tumeumbwa na roho nzuri isipokuwa mazingira ndiyo yanayotufanya wengine tukawa na roho chafu na wengine roho safi. Ndiyo, roho nzuri tulizoumbwa nazo zinachafuka. Tunakuwa ni binadamu wenye roho chafu. Na hakika, Watanzania wengi tunakufa kutokana na roho chafu, zetu wenyewe au za wenzetu.
”Mh!” Anaguna Mpoto. Ananiacha niendelee.

Maana, ni mtu mwenye roho chafu tu anayeweza kuhujumu mradi wa kuangamiza malaria inayosababisha vifo vya maelfu ya watoto na watu wazima kwa tamaa zake binafsi. Ndiyo, kuhujumu mradi wa kuzuia malaria ili apate fedha za kufanya mambo ya fahari au hata kununua uongozi wa kisiasa. Kwa mwanadamu, ni heri ufe kwa kupambana na anayehujumu mradi wa kuangamiza malaria kuliko kufa kwa malaria inayotokana na mbu anayesababisha malaria.”

Tukazidi kuzama kwenye la fikra. ”E bwana, Makambako hapa. Nafurahi kila ninapokuwa mbali na Dar es Salaam,” anatamka Mpoto.

”Kwanini unafurahi kuwa mbali na Dar?” Namwuliza Mpoto.

”Maggid, angalia nje. Hawa ndio Watanzania wanaopambana kila kukicha kwa maendeleo ya nchi yetu na kuna wachache mijini wanaodhani kuwa ni haki yao Watanzania hawa kuishi katika hali ya ufukara pamoja na rasilimali zote hizi tulizonazo.”

Kwa hiyo ndio maana umefurahi kuwa mbali na Dar?”

”Wakati mwingine ni muhimu kutoka nje ya miji mikubwa kama Dar, kwenda mbali na kuona hali halisi,” ananijibu Mpoto.

Turudi kwenye mada ya Watanzania na roho zetu chafu. Na hili lina mantiki katika kipindi hiki cha kampeni za Uchaguzi Mkuu. Nilimsimulia Mpoto kisa nilichopata kukisimulia huko nyuma. Kisa cha bwana aliyemwomba sana Mungu amsaidie. Siku moja akaambiwa; sala zako zimekwishakusikilizwa, isipokuwa, Mungu atakusaidia kwa sharti moja; kwamba kile atakachokupa wewe, basi, jirani yako atampa mara mbili yake.

Bwana yule akahitaji muda wa kwenda kutafakari kabla hajampa Mungu jibu. Akarudi na jibu; ” E Mola wangu, naomba unipe chongo, utoboe jicho langu moja. Bwana yule alikuwa tayari awe na chongo ili jirani yake awe kipofu kabisa!

Na hakika, Watanzania wa kawaida walio wengi si watu wenye roho chafu. Isipokuwa, tuna bahati mbaya ya kuwa na baadhi ya viongozi wabinafsi na wenye roho chafu huku wakilindwa na mapungufu ya kimfumo katika matendo yao maovu.

Ni viongozi ambao, kama kuna kuchagua kati ya wao kupata kimoja na wanaowaongoza kupata viwili, basi, wana hiari ya kuchagua kupata kilema cha mguu mmoja ili wanaowaongoza wawe viwete.

Ndani ya roho ya mgombea hana chema anachowatakia wapiga kura wake. Anajiangalia yeye tu. Yote hii inatokana na kukithiri kwa ubinafsi. Na mapungufu ya kimfumo nayo yanawasaidia viongozi hawa wabinafsi kutenda maovu yao kwa wananchi bila hofu. Katika kuendekeza ubinafsi wao, unaweza kabisa kuamini, kuwa viongozi hawa wanawachukia Watanzania wenzao.

Ni kwa sababu ya ubinafsi na roho zao chafu. Na anachoshindwa kuelewa kiongozi huyu anayechukia maendeleo ya mpiga kura wake ni ukweli kuwa maendeleo ya mtu huyo binafsi yatakuja kwa namna moja au nyingine kumnufaisha hata yeye na Taifa kwa ujumla. Na tuna wabunge wengi watakaoangushwa na wapiga kura wao katika uchaguzi wa Oktoba kwa sababu wameshindwa hata kuficha makucha yao ya ubinafsi.

Kwa wabunge hawa, miaka mitano ya kukaa bungeni imewaletea neema kubwa wao binafsi huku majimbo yao bado yakiwa nyuma sana kimaendeleo. Lakini, kuna wabunge ambao, wamejitahidi sana. Na mifano ya juhudi zao za kuwaletea maendeleo watu wa majimbo yao inaonekana.

Hawa watatendewa haki, maana, wananchi wa majimbo husika wanawajua na wanajua waliyoyafanya kwa maendeleo ya majimbo yao. Hakika, wananchi wamechoka kuvutwa nyuma kimaendeleo. Kuvutwa nyuma kunakosababishwa na baadhi ya viongozi waliowapa dhamana za uongozi.

Mathalan, katika nchi hii hutokea anayehusika na kuwasaidia Watanzania wenzake kupata nafasi za kwenda kusoma nje ya nchi akatoa nafasi hizo kwa upendeleo. Ataanza na familia yake, ndugu na atamalizia na jamaa na rafiki zake. Wakisha hao yuko tayari nafasi hizo zibaki tupu kuliko kuwasaidia Watanzania wengine.

Kuna vyuo vya humu duniani utakuta wamejaa Waafrika kutoka nchi nyingine, iwe Ghana, Nigeria, Kenya na kwingineko. Lakini utashangaa ni kwa nini idadi ya Watanzania ni ndogo sana au hawako kabisa kwenye vyuo hivyo. Tofauti hapa ni ukweli kuwa wenzetu katika mataifa mengine wanasaidiana sana katika kupashana taarifa juu ya kuwapo kwa vyuo hivi na namna ya kupata nafasi hizo. Mathalan, nchi kama Ghana ikitengewa nafasi 50 kwa mwaka katika vyuo vya nchi ya kigeni, basi idara husika katika Ghana itahakikisha nafasi hizi zinajazwa.

Tuna haja ya kufanya jambo moja muhimu kwa sasa; tujenge moyo wa uzalendo na utaifa. Tuipende nchi yetu. Tupendane kama Watanzania. Ubinafsi uliokithiri na kuwa na roho chafu, hususan, kwa baadhi ya tuliowapa dhamana za uongozi unatuweka mahala pabaya kama Taifa. Huko tunakokwenda tatizo hili litatutafuna. Ndiyo, roho zetu chafu zitasababisha Taifa kuangamia. Mtaona ishara…

1 comment:

  1. Sasa kuna kosa moja sisi watanzania tunalifanya, kwa kweli tunaamini kuwa mhindi na mzungu ndio watatuokoa kutokana na umaskini.UONGO. hawa watu wanafurahia maisha yao na kutupumbaza sisi, wanafurahia raslimali zetu huku tukifikiria wnaleta utajiri humu, ushoga ulitoka wapi kwenye jamii yetu? tuamke jamani, tanzania ni ya mtanzania yakhe! waende sasa!

    ReplyDelete