Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Thursday, September 23, 2010

Ban Ki Moon Amteua Mkapa Kuongoza Jopo Sudan Kusini


Mwandishi Maalum

New York- Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon amemteua Rais
Mstaafu wa Tanzania Benjamin William Mkapa ,kuongoza jopo la tume ya watu
watatu itakayoangalia mchakato wa kura za maoni Sudan Kusini na Jimbo la
Abyei.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Umoja wa Mataifa ( jana jumatano),
uteuzi huo unatokana na maombi yaliyotolewa pande mbili zinazounga mkono
makubaliano ya amani ya kudumu nchini Sudan.Pande hizo ni Serikali ya Sudan
na Kikundi cha People’s Liberation Movement.

Wengine walioteuliwa ni aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Ureno,
Bw. Antonio Moteiro na Bw. Bhojraji Pokharel Mwenyekiti wa zamani wa Tume
ya Uchaguzi nchini Nepal.

Akizungumzia uteuzi huo, Ban Ki Moon anasema ana imani kwamba tume
aliyoiteua itasaidia kufanyika kwa kura hiyo ya maoni itakayozingatia matakwa
ya watu wa Sudan Kusini na Jimbo la Abyei

Jukumu kubwa la tume hiyo pamoja na mambo mengine ni kufanya ziara za mara
kwa mara nchini Sudani katika kipindi chote cha mchakato wa kuelekea kura za
maoni. Upigaji wa kura za maoni unatarajiwa kufanyia mwezi Januari 2011

Tume hiyo pia inatarajiwa kukutana na kushirikiana na pande zote zinazohusika
katika mkataba wa amani, tume inayoratibu kura ya maoni, jumuia za kiraia na
makundi ya waangalizi wa kura hiyo.

Pamoja na kutoa taarifa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, tume hiyo
itafuatilia kwa karibu mchakao mzima wa kura za maoni na pia masuala ya
kisiasa na hali ya usalama.

Tume itatakiwa pia kufanya kazi ya kuhakikisha inaimarisha imani ya mchako
wa kura za maoni, kuhakikisha na kuzitaka pande husika na viongozi kuchukua
hatua za pamoja za kutatua matatizo yoyote au migogoro itakayojitokeza.

Wananchi wa Sudan Kusini watapiga kura yao ya maoni kuamua iwapo wajitenge
na Serikali ya Khartoum ,wakati wananchi wa Jimbo la Abyei linalogombaniwa
na pande zote mbili ,wao watapiga kura ya kuamua wajiunge na upande upi
iwapo Sudan Kusini itajitenga na Kaskazini.

Upigaji wa kura ya maoni ni miongoni wa mabadiliko yaliyofikiwa katika Mkataba
wa Amani wa mwaka 2005(CPA), uliomaliza vita vya zaidi ya miongo miwili nchini
humo. Aidha kura hiyo ni muhimu sana kwa mstakabali wa nchi yote ya Sudan.

No comments:

Post a Comment