Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Thursday, September 23, 2010

Swebe ainyemelea siasi

Unamkumbuka toto tundu Swebe, yule aliyekuwa akiigiza enzi zile na kina Kipemba, Bi Staa, Kibakuli, Mhogo Mchungu, Kingwendu, Bi Hindu, Sandra, Nina, Nora na wengine wengi?Adam Melele ndiyo jina lake halisi.

Mara ya mwisho alionekana kwenye maigizo ya kundi la Kaole Sanaa Group mwaka 2004 na tangu wakati huo amekuwa akionekana kwenye filamu mara moja moja tofauti na wasanii wenzake kama Ray, Kanumba, Johari na wengine ambao huonekana katika filamu mpya kila kukicha.

Swebe amezungumza na kueleza sababu zilizomfanya asiuze sura mara kwa mara kama wafanyavyo wakongwe wenzake.


"Hivi sasa nafanya kazi za kijamii, niliajiriwa katika kampuni ya Experimental Marketing kama mhamasishaji juu ya ugonjwa wa Ukimwi kwa vijana, sikuweza kupata muda wa kufanya kazi ya sanaa ingawa pia nilikuwa nikiifurahia hii kazi ya uhamasishaji kutokana na ukweli kwamba vijana wenzetu wengi wamemalizwa na gonjwa hili" alisema.

Msanii huyo alisema baada ya kufanya kazi hiyo kwa miaka kadhaa sasa ameamua kurudi kwenye sanaa na sasa amekuja kuwasaidia wasanii wachanga kwa kuandaa shindano la IBUA Film Star Tanzania.

" Unapozungumzia sanaa ya maigizo nchini unakuwa kama unawazungumzia watu fulani tu ambao wamelishikilia soko hili, mimi nimekaa pembeni na kuona kuwa kwa mtindo huu soko letu halitakuwa tunahitaji kuwa na damu changa itakayochangamsha soko,

Ipo siku wateja wetu watachoka kwa kuwa watu ni wale wale na vitu vinavyozungumziwa kwenye filamu ni vile vile, tunawahitaji watu wengine watakaoleta changamoto mpya kwenye soko hili" alisema .

Swebe alisema yeye kama muasisi wa shindano la IBUA na mkongwe wa sanaa ya maigizo nchini anaamini watu wachache hawawezi kuleta mabadiliko lakini uzoefu wao utaendelea kutumika siku zote.

"Kwa kutumia uzoefu wangu nimeanzisha shindano hili lakini nahitaji mawazo ya wakongwe wenzangu ili tufanikishe zoezi hili kwa kuwa litatunufaisha wote, soko la filamu Tanzania likikua sitafanikiwa peke yangu bali wote tuliomo kwenye jahazi hili" alisema.

Wakati akiendelea na mikakati ya kuipeleka sanaa ya filamu mbele, Swebe pia amejiingiza kwenye siasa, alipokuwa anatema cheche alikuwa mbioni kuelekea kwenye kampeni huko Magomeni ambapo anagombea Ujumbe wa Serikali za Mitaa katika mtaaa wa Idrisa.


alipokuwa jaji kwenye IBUA Film Star
"Nikimalizana na wewe naelekea kwenye kampeni, nataka kuwatumikia wananchi wangu ambao kwa kweli wamekuwa wakiniunga mkono sana kwenye sanaa, sasa umefika wakati wa kuwalipa fadhila kwa kuwasimamia na kuwatetea iwapo nitachaguliwa hapo kesho" alisema Swebe.

Miaka miwili iliyopita Swebe alikuwa akionekana na kundi la Wanaume Family wakati ule halijagawanyika, akizungumzia uwepo wake kundini humo alisema ilikuwa na lengo la kuwapa kampani washkaji zake.

"Mimi sio muimbaji nilikuwa nao kama marafiki ambao tulikuwa tukishauriana mambo mengi, lakini sasa nimetingwa na shughuli nyingine nyingi ndio maana sionekani tena kwenye kambi hizo ambazo sasa zinekuwa mbili" alisema.

Kila la kheri Swebe

No comments:

Post a Comment