Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Wednesday, September 8, 2010

Mrema azungumzia kazi ya kubeba zege


Mgombea ubunge kupitia tiketi ya Tanzania Labour Party (TLP), Agustine Lyatonga Mrema.
MGOMBEA ubunge kupitia tiketi ya Tanzania Labour Party (TLP), Agustine Lyatonga Mrema katika jimbo la Vunjo Moshi Vijijini, amesema kwamba kazi ya ubunge siyo sawa na kazi ya kubeba zege ambayo itawahitaji vijana na siyo watu wazima kama yeye.

Mgombea huyo aliyasema hayo katika kipindi cha Mchakato Jimboni kinachorushwa na Runinga ya TBC1 kilichofanyika Chuo cha Ualimu Marangu hivi karibuni ambapo Mrema aliulizwa swali na mwananchi mmoja aliyetaka kujua kutokana na umri wake mkubwa na madai kwamba ni mgonjwa, je ataweza mikikimikiki ya kuwahudimia wananchi hao vyema kama wakimpa nafasi ya kuwa mbunge.

“Bungeni hatuendi kubeba zege,” alianza kujibu Mrema na kuwafanya watu waliohudhuria mdahalo huo kulipuka kwa vicheko na kuendelea kutamba kwa kusema kwamba yeye anaijua kazi hiyo vizuri sana tofauti na wagombea wengine kwa kuwa aliwahi kuwa Mbunge wa jimbo hilo kwa kipindi cha miaka 10 hivyo anapaswa kupewa kura za wananchi wa jimbo hilo la Vunjo.

“Watu wanasema sijui Mrema anaumwa, mtu huwezi kukwepa kuumwa hata Dk. Slaa (Dkt. Willibrod Slaa mgombea urais wa Chadema) aliumwa pale alipoanguka bafuni na kuumia mkono, sijui nini si mnaniona au kama mnaona mimi ni mgonjwa muulizeni mke wangu kama kweli mimi ni mzima au mgonjwa…” alisema Mrema na kumfanya mwendesha kipindi hicho Shaaban Kissu kumkatisha kwa kumwambia kuwa inatosha.

Mbali na Mrema wagombea wengine waliojitokeza katika mdahalo huo ni pamoja na John Mrema wa Chadema na Crispine Robert Meela wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao nao kama ilivyokuwa kwa Mrema walipata fursa ya kutangaza ilani za vyama vyao.

No comments:

Post a Comment