Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Thursday, September 23, 2010

Wanasiasa waongo, wanaichezea Mahakama

MAJAJI na mahakimu wamekiri kutofahamu kabisa sheria za uchaguzi hivyo kusababisha baadhi ya wanasiasa kuzichezea mahakama kwa kuwawekea wenzao pingamizi ambazo baadaye zinabainika kuwa za uongo, imeelezwa.

Pamoja na kutakiwa kuzisoma kwa kina sheria hizo, wameelezwa kuanza kuwachukulia hatua baadhi ya wanasiasa, kwa kuwafungia kupiga au kupigiwa kura kwa miaka mitano, kwa mujibu wa sheria endapo watabainika kutoa ushahidi na pingamizi za uongo mahakamani.

Jaji Mkuu Augustino Ramadhani, alisema hayo jana, Dar es Salaam wakati akifungua warsha ya siku tatu kwa mahakimu wafawidhi wa mikoa yote nchini iliyoandaliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kuhusu Uchaguzi Mkuu.

Katika hotuba yake, alikiri kuwa majaji na mahakimu wengi hawazijui sheria za uchaguzi na kwamba hali hiyo imesababisha watu kuichezea Mahakama, jambo linalopaswa kukomeshwa haraka.

“Kwa mfano wa Jimbo la Mwibara, waliwahi kukaa bila Mbunge kwa miaka minne, kila aliyeshinda aliwekewa pingamizi, sasa watu hawa wanakuja wanaapa mahakamani kuwa watatoa ushahidi wa kweli tena kweli tupu, lakini kumbe ni uongo, hili linabainika baadaye wakati wananchi wameshateseka,” alisema Jaji Mkuu na kuongeza:

“Sheria imeipa mamlaka Mahakama kuwafungia watu wa namna hii kupiga au kupigiwa kura kwa miaka mitano, na hili linapaswa kutekelezwa, maana watu wanachezea Mahakama, watu wanaapa kwa Biblia na Kurani, lakini kumbe wanasema uongo.”

Alisema mtu anakuja mahakamani kutoa ushahidi, kwamba alipewa rushwa na mgombea fulani na kuapa, lakini anasahau kwamba naye ni mtuhumiwa kwa mujibu wa sheria, ingawa ni shahidi.

Alisisitiza kuwa, mahakimu wanapaswa kuzisoma sheria ili kutatua matatizo ya namna hiyo ambayo ni mengi mahakamani.

Kwa upande wao, washiriki walikiri pia kuwa hawazijui sheria za uchaguzi kwa kuwa hawafundishwi vyuoni na kuongeza:

“Binafsi naona ni wakati muafaka UNDP wanatupiga msasa, ingawa wamechelewa, lakini si mbaya kwa kuwa tulio wengi hatuzijui kabisa hizi sheria za uchaguzi,” alisema Richard Kabate, Hakimu Mfawidhi wa Mkoa wa Morogoro.

Kabate alishauri semina hiyo isiishie kwa mahakimu wa ngazi za mkoa, bali iende mpaka wilayani, kwa kuwa sheria inatoa mamlaka kwao pia kusikiliza kesi zitokanazo na uchaguzi wa kisiasa sambamba na kuwataka mahakimu waliopata mafunzo, kuyaendeleza kwa wenzao, ili matunda ya semina hiyo yaonekane.

Awali Mkurugenzi wa UNDP nchini, Philippe Poinsot, alisema ni muhimu mahakimu kuelewa vyema namna ya kushughulikia mashauri yatokanayo na uchaguzi, kulingana na sheria zake, kwani itasaidia kuepuka vurugu na kuwezesha kushughulika na masuala ya maendeleo na mapambano dhidi ya umasikini nchini.

No comments:

Post a Comment