Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Saturday, June 12, 2010

Enhe elezea kwanini ulivamia uwanja wa Taifa na kumpa Kaka mahug ya kutosha!


Siku chache baada ya Shabiki wa soka Nagari Kombo (21) kuvamia katikati ya wanja la Taifa, jijini Dar es Salaam wakati mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, na Brazil ikiendelea, ameanika sababu za kufanya hivyo.

Alichofanya kijana huyo akiwa peku huku akionekana kama mtu aliyepagawa, alichomoka kutoka upande wa mashariki mwa uwanja na kumfuata Kaka kisha kumkumbatia huku Kaka naye akifanya hivyo na kumpigapiga mgongoni kuashiria kupokea salamu.

Huku umati uliofurika uwanjani ukipigwa butwaa usijue kulikoni, kijana yule akionekana hana madhara, aliendelea na safari yake huku akishangilia kufanikiwa lengo lake kabla ya kudakwa na askari polisi akiwa nje ya uwanja.

Licha ya kuwekwa chini ya ulinzi, kilichoonekana kwa Kombo, ni kufurahia kile alichokifanya cha kumfuata Kaka na kumkumbatia, ingawa sasa amejikuta akiangukia mikononi mwa Jeshi la Polisi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Kanda Maalumu ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Naibu Kamishna (DCP), Suleiman Kova, kabla ya mechi hiyo, Kombo alijiwekea nadhiri kwamba Brazil watakapokuja nchini, atahakikisha anagusana na Kaka.

Kova alisema kwa mujibu wa kijana huyo, kwa vile alijua adha ambayo ingempata kwa kitendo kile, kabla hajaingia uwanjani, alisaula pochi, viatu na simu ya mkononi na kutekeleza azma yake.

Kijana huyo amewaeleza polisi kuwa hakuwa na nia mbaya zaidi ya kutimiza azma yake ili iwe kumbukumbu katika maisha yake.

“Amesema isingekuwa rahisi kwake (Kombo) kukubali Kaka ambaye amekuwa akimwona akicheza kupitia runinga aje katika ardhi ya Tanzania na kuondoka bila yeye kushikana naye,” alisema Kova.

Kijana huyo aliyetoa maelezo hayo katika Kituo cha Polisi cha Chang’ombe, hadi jana alikuwa anashikiliwa kwa kosa la jinai la kuingia sehemu isiyoruhusiwa (Trans-pass).

Kova alisema shabiki huyo alitumia mbinu ambayo askari asingeweza kugundua kwani wakati anashuka, alionekana kama anayekwenda kujisaidia, lakini ghafla aliruka uzio na kwenda uwanjani kutimiza lengo lake.

Hata hivyo, Kova alisema si tukio la ajabu kwani hutokea hata katika nchi nyingi licha ya ulinzi kutokana na wahusika kutumia mbinu kali katika kufanikisha malengo yao kama alivyofanya.

“Jamani ulinzi katika mechi hiyo uliimarishwa vizuri, kwa aina ya kosa la Kombo, lisingeweza kuzuilika kutokana na kutumia mbinu kali za kuhakikisha anamfikia Kaka,” alisema Kova.

Kova alitolea mfano wa tukio kama hilo katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Arsenal na Barcelona ambapo shabiki mmoja wa Arsenal alivamia uwanja na kwenda kumfunika Thiery Henry kwa bendera.

Akirejea katika tukio ya Kombo, alisema wakati askari wakiwa wanaagalia juu ya usalama wa jukwa la juu alianza kutoa viatu na pesa kwa kukabidhi marafiki wengine wakijua midadi ya soka imempanda na kumuacha na utaratibu wake.

Kova amesema ingawa ni tukio la kishabiki zaidi, lakini Jeshi la Polisi halina budi kufanya kazi yake kwa vile ni kosa ambalo pia liliwanyima haki wote waliokuwa wakimfuatilia Kaka uwanjani muda ule.

Brazil imerejea nchini Afrika Kusini tayari kwa kampeni ya kusaka ubingwa wa sita wa Kombe la Dunia ambapo ikiwa katika kundi G, itaanza kampeni Juni 15 kwa kukipiga na Korea Kaskazini.

Brazil iliyopangwa kundi hilo lenye pia timu za Ivory Coast na Ureno, mechi ya juzi dhidi ya Stars, ni ya sita kwake katika ardhi ya Afrika huku Zimbabwe iliyocheza nayo Juni 2, ikiwa ya tano.

No comments:

Post a Comment