Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Friday, June 11, 2010

Sawa Mheshimiwa yuko salama ila magari yanahitaji kazi ya ziada!


IKULU imewatoa wasiwasi wananchi kuhusu usalama wa Rais Jakaya Kikwete na kuwahakikishia kuwa mkuu wa nchi yuko katika mikono ya watu makini, salama na wazalendo wanaoifahamu kazi yao.


Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salvatory Rweyemamu, wakati akifafanua kuhusu tukio la magari matano yaliyokuwapo kwenye msafara wa Rais mkoani Kilimanjaro kupatwa na hitilafu na kushindwa kuwaka wakati wa ziara yake wiki hii.

Akifafanua kuhusu tukio hilo lililotokea Juni 8, mwaka huu, alisema sehemu ya magari ambayo ilikuwa yatumike kwenye msafara huo, yakiwa katika utaratibu wa maandalizi ya kumpokea Rais Kikwete katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), yalipelekwa katika kituo cha mafuta cha Rafiki.

“Baada ya kujazwa mafuta magari matatu kati ya hayo matano, yalikataa kuwaka, baada ya kuona hivyo, uamuzi ulichukuliwa wa kutoyawasha kabisa yale magari mengine mawili,” alisema Rweyemamu.

Hata hivyo, alisema kituo kilichotumika ni moja ya vituo ambavyo vimekuwa vinatumiwa kujaza mafuta ya magari ya Rais siku nyingi na kwamba uamuzi wa kuyajazia mafuta magari hayo katika kituo hicho haukuwa wa kushtukiza ama kubahatisha.

“Ukweli ni kwamba uamuzi wa wapi pa kujaza mafuta magari ya Rais, si wa madereva, bali huanzia ngazi za juu,” alifafanua.

Alisema kinachofahamika ni kwamba wakati magari hayo yanaingia kujazwa mafuta kituoni hapo, yalikuwa mazima, imara na salama kwa ajili ya kumpokea Rais Kikwete aliyekuwa anatokea Dar es Salaam na kwamba tatizo lilianza baada ya kujazwa mafuta hayo.

Hata hivyo, Rweyemamu alisema pamoja na hitilafu hiyo, msafara wa Rais ulipokelewa kama ilivyopangwa bila tatizo lolote kutokana na misafara ya aina hiyo mara zote huwa na mipango mbadala ya usafiri yenye kiwango cha juu cha usalama.

Alisema magari yaliyopata hitilafu hayakutumika kabisa katika msafara huo kwa kuwa yalikuwa yanasafishwa ambapo baada ya kusafishwa na kuwekewa mafuta mengine, yaliwashwa na kuwaka na yapo safarini kurejea Dar es Salaam.

“Uchunguzi wa tukio hili zima kwa sasa uko mikononi mwa vyombo vya usalama ikiwamo Polisi na Mamlaka ya Usimamizi wa Nishati na Maji (EWURA) na wakikamilisha uchunguzi wao, wananchi watajulishwa nini hasa kilitokea,” alisema.


Alisema tukio hilo haliathiri kitu chochote katika ziara hiyo na wala halikusababishwa na uzembe na kuhusu usalama wa Rais, hauna shaka yoyote na uko mikononi mwa watu wa kuaminika

No comments:

Post a Comment