Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Monday, June 14, 2010

Huu ndio mwisho wa Kero za mikopo kwa wanafunzi- JK


FEDHA za kukopesha wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka ujao wa fedha unaoanzia Julai mwaka huu, zitatengwa maalumu ili zipatikane wakati zinapohitajika na kukomesha uchelewaji wa fedha hizo.

Aidha, mwakani serikali inajipanga kuja na mkakati mwingine mahususi ambao wanafunzi wanaotaka kukopa, watakopeshwa na kujiwekea deni bila kujali uwezo wa wazazi wao.

Rais Jakaya Kikwete alisema hayo jana mjini hapa baada ya risala la wanafunzi wa elimu ya juu wa Mkoa wa Dodoma, kusisitiza matatizo wanayopata wanafunzi hao katika upatikanaji wa mikopo hiyo.

Katika risala hiyo, iliyosomwa na mmoja wa wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Egla Mamoto, wanafunzi hao pamoja na kumpongeza Kikwete kwa wazo lake la kujenga chuo hicho, lakini walisisitiza tatizo la kupata mikopo elimu ya juu.

“Tuko katika mtihani, lakini kwa kuzingatia kuwa wewe ndiyo chimbuko la elimu yetu, tumetenga muda kuja hapa,” alisema Mamoto na kushangiliwa.

“Maandamano haya ni kielelezo cha mapenzi yetu kwako na tunaunga mkono uwe mgombea pekee 2010 na tunazo sababu,” alisema.

Alitaja miongoni mwa sababu hizo kuwa ni utekelezaji makini wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2005 hasa katika elimu ambayo imewagusa na kusimamia wazo lake la ujenzi wa UDOM.

“Ulitoa wazo, ukalisimamia, ukajenga chuo kikuu, kwa hili usiseme wacha sisi wenyewe tunaonufaika tukusemee. UDOM ina hadhi ya kimataifa, je kama si wazo lako, leo hii tungekuwa wapi?” Alihoji mwanafunzi huyo na kushangiliwa na wenzake.

Alisisitiza pamoja na mafanikio hayo wanafunzi wanapata matatizo ya kupata mikopo.

Akijibu hoja hiyo ya mikopo pamoja na nyingine zilizoainishwa katika risala hiyo, Rais Kikwete alisema nia ya kuanzisha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ilikuwa njema na wataiendeleza.

Alisema tatizo la kuchelewa kwa fedha za mikopo lilitokana na fedha hizo kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kabla ya kufika HESLB.

Kutokana na tatizo hilo, ambalo wakati mwingine wizara hiyo ilizitumia fedha hizo, sasa kutaundwa mfumo ambao fedha za mikopo hazitapitia wizarani, badala yake zitawekwa maalumu ziwe tayari kwa matumizi ya wanafunzi wakati wowote.

Mbali na mfumo huo, mwakani kutaundwa mkakati wa kukusanya zaidi ya Sh bilioni 700 kwa wadaiwa vyuo vikuu, ili wanafunzi wa elimu ya juu watakaohitaji mikopo, wapatiwe bila kujali uwezo wa wazazi.

Kuhusu ujenzi wa UDOM, Rais Kikwete alikiri kuwa ujenzi wa chuo hicho haukuwa katika Ilani ya CCM ya 2005, bali waliibadilisha ili kuanza ujenzi wa chuo hicho.

Alifafanua kuwa “katika Ilani imendikwa tutapanua elimu ya juu, lakini wao wakabadilisha kidogo na kuweka, tutajenga chuo kikuu.”

Kauli hiyo ya Rais, imekubaliana na hoja ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, aliyoitoa wiki iliyopita kwamba UDOM haiko katika Ilani ya CCM.

No comments:

Post a Comment