Habari mbalimbali toka pande za bongo bila kusahau matukio mbalimbali yanayorindima pande zote za dunia
Psquare Ft. J.Martins- E No Easy
Thursday, June 3, 2010
Kadi zawaponza viongozi CCM!
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam kimeanza kuwakamata watendaji wake wanaodaiwa kugawa kadi za uanachama wa chama hicho isivyo halali kwa lengo la kuwapitisha katika kura za maoni wagombea ubunge.
Watendaji waliokamatwa ni Katibu wa Kata ya Kivukoni, Mohamed Mponda ambaye kwa sasa anashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Pangani wilayani Ilala na Katibu wa Tawi la Balozi Msolomi katika Kata ya Mwananyamala wilayani Kinondoni, Charles Zyambo aliyefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Mei 28, mwaka huu.
Akifafanua zaidi juu ya matukio hayo, Katibu wa Mkoa wa chama hicho, Kilumbe Ng’enda alisema kamati za maadili zinafanya ukaguzi katika matawi yote 648 yaliyopo katika kata zote 73 za Mkoa wa Dar es Salaam kubaini utoaji holela wa kadi za wanachama wapya unaoambatana na rushwa.
Ukaguzi huo umekuja baada ya Aprili mwaka huu, chama hicho kupokea taarifa za utoaji holela kadi pamoja na kuzihamishia mikoa mingine.
Katika ukaguzi huo, kata za Tabata, Kitunda na Ilala zimebainika kutokuwa na kasoro zozote na ukaguzi huo unaendelea.
“Ilibainika Katibu wa Tawi la Balozi Msolomi alipewa kadi 120 Juni 11, mwaka jana, lakini hadi Mei mwaka huu ni wanachama 35 tu waliopata kadi na wengine wanaendelea kusubiri ambapo kadi 85 hazijulikani alizipeleka wapi kwani ofisini kwake hazipo na zilionekana amezipeleka mkoa mwingine,” alifafanua Katibu huyo.
Kutokana na hilo, alisema Katibu huyo alifikishwa Kituo cha Polisi Oysterbay na Mei 28, alifunguliwa mashitaka katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, huku Katibu wa Kata ya Kivukoni, Mponda wakati akihojiwa na maofisa maadili alitoroka na kwa siku tatu hakuwepo nyumbani kwake ndipo chama hicho kilipotoa taarifa polisi waliomkamata juzi saa 12:30 jioni na kwa sasa anashikiliwa kituoni.
“Mponda alikutwa amefuta majina ya wanachama halali kwa wino mweupe na kuandika majina mengine na mmojawapo alikuwa ameshakufa.
Alipewa kadi zaidi ya 160 na kadi 83 kati ya hizo, hazijulikani zilipopelekwa”, alieleza Ng’enda.
Alisema wamebaini kadi hizo mbali na kuuzwa isivyo halali, pia zinahamishwa kwenda mikoa mingine na kutoka mikoani zinaletwa Dar es Salaam; lengo ni kupewa wanachama wapya watakaowapigia kura wagombea wao.
Kwa mujibu wa taratibu, mwanachama akishaomba uanachama hapewi kadi hadi apitishwe na Kamati ya Siasa ya Tawi na kulipa ada ya Sh 300.
Katika utaratibu wa mwaka huu, wanachama wote hai wa CCM watawapitisha wagombea katika kura za maoni tofauti na miaka ya nyuma ambapo wajumbe wa Mkutano Mkuu pekee wa kata ndiyo waliokuwa wakiwapitisha wagombea ubunge.
“Nawaomba viongozi hasa wa kuchaguliwa watuachie tufanye kazi zetu, mimi ndio Mkurugenzi wa Uchaguzi Mkoa wa Dar es Salaam…tukisikia taarifa za kiongozi yeyote amehifadhi kadi tutakwenda kumpekua na tukimkuta nazo, atafikishwa mahakamani”, alionya Katibu wa Mkoa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment