Habari mbalimbali toka pande za bongo bila kusahau matukio mbalimbali yanayorindima pande zote za dunia
Psquare Ft. J.Martins- E No Easy
Wednesday, June 16, 2010
SAKATA LA OFISI KUCHOMWA MOTO MTANDAO HUU WABAINI SIRI NZITO,VIONGOZI WATATA WAKAMATWA
IMEBAINIKA kuwa ukimya wa tume iliyoundwa na mkuu wa wilaya ya Mufindi Evarita Kalalu kuchunguza tuhuma za viongozi wa serikali ya kijiji cha Igowole wilayani humo juu ya ufujaji wa mali za kijiji ndio uliopelekea hujuma kuchomwa moto kwa ofisi hiyo ya na nyaraka zote
Kuchomwa moto kwa ofisi hiyo ya serikali kunadaiwa ni kutokana na mkuu wa wilaya ya Mufindi Evarita Kalalu kuchewesha majibu ya tume aliyokuwa ameiunda kwa ajili ya kuchunguza ufisadi uliokuwa umefanyika katika kijiji hicho na viongozi wa serikali ya kijiji kwa kuuza miti ya kijiji kinyemela na fedha kuzitumia wao katika matumizi binafsi
Akizungumza namtandao huu juu ya tukio hilo mwenyekiti wa tume ya mkuu wa wilaya kijijini hapa Hosea Kyando alisema kuwa kabla ya watu hao wasiofahamika kuchoma moto ofisi ya kijiji juzi usiku mchana waliweka vipande vya sabuni katika mlango wa ofisi ya kaimu afisa mtendaji wa kijiji hicho ambaye ana wiki moja pekee toka aripoti kijijini hapo
Alisema kuwa kutokana na wananchi wa kijiji hicho kuukataa uongozi wa kijiji chini ya mwenyekiti wake Idphonce Kafuka ,mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mufindi alituma wakaguzi kwa ajili ya kukagua hesabu za kijiji hicho ambazo zilikuwa zikilalamikiwa na wananchi hao kiasi cha kufanya maandamano makubwa kuwataka viongozi wote wa kijiji kujiuzulu.
Hata hivyo viongozi hao hawakuweza kujiuzulu zaidi ya mkuu wa wilaya hiyo kuingilia kati suala hilo kwa kuunda tume ya kuchunguza malalamiko ya wananchi tume ambayo iliwasilisha ripoti yake ndani ya muda uliopangwa japo hadi sasa ni siku 14 zimepita bila mkuu wa wilaya kufika na kutoa ripoti ya uchunguzi wa tume hiyo kama alivyoahidi.
Hivyo alisema kuchelewa kutolewa kwa majibu ya tume hiyo ndiko kulikowakwaza zaidi wananchi hao ambao walilazimika kufunga safari hadi kwa mkuu wa mkoa wa Iringa Mohamed Abdulaziz kufikisha malalamiko yao na kuomba tume ya mkuu wa wilaya kutoa majibu yake.
"Hapa kuna mawili yawezekana ni viongozi wanaotuhumiwa wameamua kufanya hujuma ya ofisi ili kupoteza ushahidi...ama yawezekana ni wananchi wameamua kuchoma moto ofisi baada ya kuchukizwa na ukimya wa mkuu wa wilaya dhidi ya tume yake"
Pia alisema wakati moto huo ukiteketeza ofisi juzi usiku kegere iligongwa na wananchi wote waliweza kufika kuzima moto huo ila viongozi hao wa serikali ya kijiji ambao wamekuwa wakipingwa na wananchi hawakuweza kufika hata mmoja .
Mwenyekiti huyo alisema kuwa hadi sasa tayari askari polisi wamefika katika kijiji hicho kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo japo na viongozi watatu akiwemo mwenyekiti na afisa mtendaji wamekamatwa na polisi kuhusiana na tukio hilo.
Mkuu wa wilaya ya Mufindi Bibi Kalalu alipoulizwa na mwandishi wa habari hii juu ya tume hiyo kuundwa na kushindwa kutolewa majibu kwa wakati alisema kuwa kwa sasa yupo jijini Dar es Salaam kwa matibabu na hawezi kulizungumzia zaidi suala hilo kutokana na matatizo ya kifanya yanayomsumbua huku mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo ya Mufindi Limbaksye Shimwela hakuweza kupatikana kuzungumzia tukio hilo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment