Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Wednesday, April 7, 2010

Kesi ya Richmond hiii hapa


Mitambo ya Richmond.

Kesi ya Kampuni ya Richmond dhidi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) imehamishiwa Dubai na imepangwa kusikilizwa kuanzia Jumatatu ijayo.

Mwanasheria wa Tanesco, Subira Wandiba, jana aliiambia Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC) kuwa kampuni hiyo imeihamishia kesi hiyo Dubai kwa kuhofia mmoja wa wamiliki wa Richmond kukamatwa nchini. Hata hivyo, Wandiba alisema kampuni hiyo inaidai Tanesco Dola za marekani milioni 109 na iwapo itashindwa kesi italazimika kuilipa Tanesco kiasi hicho cha fedha.

Wakati huo huo, mwanasheria huyo alisema mitambo ya Kampuni ya Dowans imeuzwa kinyemela kwa kampuni moja ya kigeni, lakini Tanesco limeweka pingamizi mahakamani kuzuia mitambo hiyo isiondolewe nchini hadi kesi kati ya Dowans na Tanesco itakapomalizika.

Mwanasheria huyo aliiambia kamati hiyo kuwa kesi kati ya Tanesco na Dowans itasikilizwa nchini Ufaransa Juni mwaka huu.Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe, alihoji sababu za Tanesco kutoinunua mitambo ya Dowans ili wakati wa malipo serikali iweze kulikata deni hilo.

Akijibu hoja hiyo, Wandiba alisema wakati wa majadiliano Dowans walipinga.

Wakati huo huo, Tanesco imeipa kampuni ya Deloitte & Touche ya Afrika Kusini kazi ya kukagua Dola milioni 7.9 ambazo zilitumiwa na kampuni ya Songas kufanya upembuzi yakinifu baada ya kubainika kuwa fedha hizo ni nyingi kulinganisha na kazi iliyofanyika.

Kaimu Afisa wa fedha wa Tanesco, Anetha Chengala, alisema kampuni hiyo ilianza kazi tangu mwezi uliopita. Alisema pia kuwa wamemuomba CAG kukagua fedha za Songas ili kubaini mwenendo wa biashara wa kampuni hiyo.

Baada ya ufafanuzi huo, Zitto alisema kamati itamwandikia barua CAG kuhusu umuhimu wa kufanya ukaguzi huo ili Songas ianze kulipa kodi.

Kamati ilishangaa kuona Songas inalipwa Sh. bilioni sita kwa mwezi kama wakati inaiuzia Tanesco umeme wa Sh. bilioni mbili hadi tatu kila mwezi.

No comments:

Post a Comment