Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Monday, April 12, 2010

RPC anusurika kutekwa Mwanza

KAMANDA wa Polisi mkoani Mwanza, Simon Siro jana amenusurika kutekwa na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi ambao walikuwa wamemtegea mawe barabarani.

Mtego huo uliwekwa usiku wa kuamkia juzi majira ya saa sita wakati Kamanda huyo alipokuwa katika doria ya usiku akitokea wilayani Sengerema kwenda katika kivuko cha Busisi.

Habari zilizopatikana kutoka eneo la tukio katika kijiji cha Nyitundu kata na tarafa ya Busisi, zimeeleza kwamba baada ya Kamanda Siro kukuta mtego huo alilazimika kushirikiana na askari aliokuwa nao kuyatoa mawe hayo.

“Baada ya kuyakuta mawe hayo walishuka kutoka kwenye gari na kuamua kuyasogeza mawe hayo pembeni mwa barabara na kuendelea na safari yao, lakini inavyoonekana alipatwa na wasiwasi mkubwa,” kilisema chanzo chetu cha habari kutoka katika eneo la tukio.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, baada ya kufika umbali wa kilometa mbili hivi, Kamanda Siro aliwaamuru askari wote kurudi eneo lililokuwa na mtego huo.

“Walipofika katika eneo hilo walikuta mawe waliyoyatoa barabarani yakiwa yamerejeshwa huku wakiwepo watu wawili wenye mapanga, lakini baada ya kuwaona askari walitimua mbio na askari wakiongozwa na Kamanda Siro waliwakimbiza kwa miguu na kufanikiwa kumkamata mmoja wao.

Akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu kutoka wilayani Magu ambako anahudhuria kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Kamanda Siro alithibitisha kukutana na mtego huo na kuahidi kupambana na wahalifu kwa kila kona ya Mkoa wa Mwanza.

‘Ni kweli ilitokea jana usiku (juzi) kwenye saa sita hivi…..nilikuwa wilayani Sengerema sasa nikaamua kuwachukua vijana wangu ili tufanye doria, nikapita hiyo barabara ya kwenda kwenye kivuko cha Busisi ambapo nina taarifa kwamba kuna eneo moja ambalo majambazi wanapenda sana kuteka magari pamoja na raia,” alisema Kamanda Siro.

“Cha ajabu baada ya kufika kwenye kijiji kimoja kinachoitwa Nyitundu ambapo kuna matengenezo ya barabara ya lami ambayo haijakamilika, tukakuta mawe barabarani, dereva wangu akasimamisha gari tukashuka tukayatoa, ni mawe makubwa,’’ alisema.

Alifafanua kwamba baada ya kwenda umbali kama wa kilometa mbili hivi, alimuamuru dereva wake kusimamisha gari na wakarejea katika eneo hilo kwa ajili ya kuangalia hali ya usalama.

“Nilichotaka ni kuthibitisha kama kweli yale mawe yalikuwa yamewekwa pale na majambazi, na kweli Mungu si Athumani, tulipofika tu tukakuta yale mawe yamerejeshwa barabarani na kwa bahati nzuri zaidi kukawepo watu wawili kwenye eneo lile.

“Nikaona tayari tumepata kazi ya kufanya, nikawaamuru vijana kufanya kazi ambapo nilishirikiana nao kuwakimbiza watuhumiwa hao na kufanikiwa kumkamata mmoja wao, mwingine alituponyoka,’’ alifafanua Kamanda Siro.

Baada ya kumkamata mtuhumiwa huyo, walianza operesheni usiku huo huo katika kijiji hicho kutokana na maelekezo ya mtuhumiwa ambaye walifanikiwa kumkamata ambayo yalifanikisha kuwakamata watuhumiwa wengine wanane ambao wanaendelea kuhojiwa.

Kamanda Siro ametangaza vita na watuhumiwa wote wa ujambazi katika eneo hilo ambalo linasifika kwa matukio ya utekaji wa magari ya abiria na mizigo, na amewataka watuhumiwa kujisalimisha mapema kabla ya msako mkali kuanza katika eneo hilo.

Eneo hilo limekuwa na matukio mengi ya utekaji wa magari ya abiria na yale ya mizigo na hasa malori yanayokwenda nje ya nchi kama vile Burundi, Rwanda na DRC, ambapo mara kadhaa watu wameporwa mali na fedha zao.

Tangu alipohamia mkoani Mwanza, Kamanda Siro ambaye amekuwa akiendesha operesheni za kusaka wahalifu yeye mwenyewe, amekuwa na mikakati kadhaa ya kupambana na uhalifu ambao umekithiri mkoani Mwanza na hasa ujambazi wa kutumia silaha.

No comments:

Post a Comment