Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Thursday, April 29, 2010

Trafiki sasa kumwaga kadi kama Marefa Wa soka!!


Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani jijini Dsm, imeanzisha mtindo wa kutoa kadi ya njano na nyekundu kama ilivyo kwa mchezo wa soka, kwa madereva wa daladala ikiwa ni njia ya kudhibiti uvunjaji wa sheria za barabarani.

Hadi sasa tayari madereva 70 wamepewa kadi za njano na wengine wanane wamepewa nyekundu ambapo wamenyang’anywa leseni zao kutokana na makosa hayo.

Hayo yalisemwa jana Dsm na Kamanda wa kikosi hicho cha usalama wa barabarani, Mohammed Mpinga.

“Tunatumia mtindo wa ‘yellow card’ na tayari tumeshazitoa kwa madereva 70 na wengine wanane tumewapa ‘red card’ hii ni katika kudhibiti vitendo vya kuvunja sheria za barabarani,” alisema Mpinga.

Pamoja na hayo, alikanusha madai ya madereva kuwa wakikamatwa kwa makosa ya barabarani hupelekwa moja kwa moja lupango kwa wiki mbili.

“Tunafuata sheria, akikamatwa dereva taratibu zipo za dhamana na hata akifikishwa mahakamani dhamana huwa wazi isipokuwa kwa wale ambao mahakama itakosa uaminifu kwao.”

Alisema hadi sasa madereva 21 wana kesi mahakamani na wengine 18 wamefungwa jela kwa muda wa miezi mitatu hadi sita kutokana na kuvunja sheria za barabarani ambazo ni kukatisha ruti na kutanua njia.

Kwa mujibu wa Mpinga, Polisi imejipanga kuhakikisha kuwa inadhibiti makosa ya barabarani na iko kwenye mchakato wa kuwa na kamera aina ya CCTV Dar es Salaam na barabara zote za mikoani.

“Kamera hizi zitasaidia sana kuona makosa ambayo kwa sasa tunashindwa kuyaona, hata ajali ikitokea mikoani kupitia kamera hizi tutakuwa na uwezo wa kurudisha mkanda nyuma na kuona tukio zima na hivyo kujua chanzo cha ajali hiyo bila shida,” alisema.

No comments:

Post a Comment