Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Monday, April 5, 2010

'Tatizo ni uwaziri mkuu'


KUJIENGUA kwa Mbunge wa Kishapu, Fred Mpendazoe kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwenda Chama Cha Jamii kumeelezwa kunatokana na chuki binafsi aliyokuwa nayo baada ya Rais Jakaya Kikwete kutomchagua katika Baraza lake la Mawaziri 2005.

Hayo yamebainishwa jana na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga Hamis Mngeja baada ya kupokea maandamano makubwa ya wana CCM na wananchi wa Wilaya ya Kishapu kwenye Uwanja wa CCM, Kishapu jana.

Mngeja alisema Mpendazoe amejenga chuki baada ya kujiamini kwa asilimia 100 kuwa angechaguliwa kuwa Waziri Mkuu au Waziri au Naibu Waziri.

Kiongozi huyo wa CCM Mkoa wa Shinyanga alisisitiza kuwa chuki hiyo iliongezeka zaidi baada ya Rais kufanya mabadiliko ya Baraza lake la Mawaziri na bado alimwacha tena katika nafasi zote alizokuwa anazitegemea.

Kutokana na chuki hiyo alianza kutapatapa na kujiingiza katika mambo ambayo wananchi wa Kishapu hawakumtuma.
Alisema katika kutapatapa kwake alimgeukia Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na kumshushia tuhuma nzito ikiwamo ya kutaka aondolewe kinga yake ili ashitakiwe kwa madai yaliyopo katika jimbo jingine la Kiwira ambalo lina mbunge wake wa kusemea.

Alisema kama hiyo haikutosha alivamia pia sakata la Richmond ambalo alidai halina uhusiano na Kishapu.


Akizungumzia madai ya Mpendazoe kwamba CCM imepoteza mwelekeo wake, Mngeja alisema haikupoteza mwelekeo bali yeye ndiye aliyepoteza mwelekeo, kwa kuwa hata wakati anatangaza kujiengua kutoka CCM aliamua kuwatangazia wananchi wa Dar es Salaam na kuwaacha wapiga kura wake njiapanda.

"Mimi nafikiri kutapatapa huku ni laana ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa kwa kuwa Mkapa ndiye aliyemuidhinisha kuwa mgombea pekee wa CCM jimbo la Kishapu, lakini matokeo yake yeye amemgeuka na kutaka mtu aliyemteua kufikishwa mahakamani na kushtakiwa," alisema Mngeja na kuwataka wananchi wa Kishapu kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha kutoswa na mbunge wao.


Awali kabla ya Mwenyekiti huyo wa CCM, kuhutubia wananchi wa kata 20 wa jimbo la Kishapu, walilaani kitendo cha Mbunge wao kuwatelekeza na kisha wakampongeza kwa kusoma alama za nyakati.

Walisema katika risala zao kuwa kujiondoa kwake kumekuwa nafuu kwani wameutua mzigo wa misumari waliokuwa wakiubeba kwa miaka minne sasa.

Walisema wao hawawezi kutetereka kwa kuwa CCM katika wilaya hiyo ina wanachama 42,000 wenye uwezo wa kuendeleza juhudi za kuleta maendeleo chini ya CCM.

Kwa mujibu wa mwandishi maandamano hayo yalikuwa na wananchi zaidi ya 30,000 na yalihudhuriwa na viongozi wa ngazi mbalimbali za wilaya zote nane za Mkoa wa Shinyanga wakiwamo wakuu wa wilaya wajumbe wa kamati za siasa, wajumbe wa Serikali za vijiji na kata na madiwani.
chanzo habari leo!

No comments:

Post a Comment