Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Monday, April 5, 2010

KKKT yasisitiza kukataa fedha za ‘mashoga’


KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), limesema halitapokea msaada wowote au fedha za mataifa yanayobariki ndoa ya jinsia moja badala yake wao watasimamia katika neno la Mungu ambalo linapinga vitendo hivyo.

Mkuu wa KKKT, Askofu Dk. Alex Malasusa aliyasema hayo jana katika salamu zake za sikukuu ya Pasaka iliyofanyika kitaifa katika Kanisa hilo Usharika wa Azania Front na kueleza kwamba hatavumilia kuona maovu hayo yakitendeka nchini.

“Hivi karibuni pamekuwa na maswali mengi juu ya matangazo yaliyosikika kwa masuala ya Marekani na Sweden ambao wamebariki ndoa ya jinsia moja, kwa kweli inasikitisha na hata mimi mwenyewe limeniumiza sana” alisema.

Alisema kuwa KKKT imekataa jambo hilo na wala haitalibariki na kusisitiza kwamba haliendani na biblia wala maandiko yoyote ya neno la Mungu.

“Sisi tutasimama katika neno la Mungu na ndio msimamo wetu wa Kilutheri na kama ni fedha zao wabaki nazo lakini sisi tutabaki na Yesu wetu aliye Hai,” alisema Malasusa.

Alisema kuwa KKKT itaendelea kusimama katika upendo na kuwahubiria watu waliochoka na kukata tamaa habari njema na wokovu ili wabadilike na kuendelea kuuhifadhi Ukristo siku zote.

Akizungumzia utitiri wa madhehebu Askofu huyo aliwataka waumini kutokukubali kuyumbishwa kama hawana akili badala yake wasimame imara na kupinga wanaotaka kuwapotosha.

“Sasa hivi kuna utitiri wa madhehebu lakini isiwatie hofu, pia wapo watumishi wanatumia madhehebu yao kuwahofia na kuwatumia watu kwa maslahi yao kwa kuwaatamia kama mayai… nawasihi simameni katika neno bila kuyumbishwa” alisema.

Pia aliwataka Wakristo kutumia fursa waliyonayo kutubu dhambi zao na kuihubiri kweli ya Mungu ili kujenga Taifa imara lenye amani na utulivu.
chanzo habari leo!

No comments:

Post a Comment