Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Friday, April 23, 2010

Mbunge Kimaro apatwa na kiharusi



MBUNGE wa Vunjo, Aloyce Kimaro (CCM), amepatwa na kiharusi akiwa bungeni mjini Dodoma na amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.

Spika wa Bunge, Samuel Sitta pamoja na uongozi wa Hospitali Kuu ya Mkoa wa Dodoma, wamethibitisha kuugua kwa mbunge huyo maarufu miongoni mwa kundi lililojipambanua kuwa linapambana na ufisadi.

Akizungumza jana jioni bungeni, Sitta alisema Kimaro alikuwa anajisikia vibaya tangu juzi na hivyo kupelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kabla ya kuhamishiwa Muhimbili jana.

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Philemon Saigodi alisema Kimaro alifikishwa hospitalini hapo juzi usiku na Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM).

Dk. Saigodi, alisema kwa mujibu wa Kimaro, alipatwa na matatizo kwa kuishiwa na nguvu ghafla katika mkono wake wa kulia na mguu wakati akipata chakula cha usiku.

“Alisema wakati anakula usiku, aliishiwa nguvu mkono wa kulia na mguu wa kulia, hivyo akaletwa hospitali,” alisema Dk. Saigodi na kuongeza:

“Baada ya kumpokea, nilimwita daktari bingwa wa viungo, Dk. Chaula na kumchunguza na kugundua kuwa ana tatizo kubwa zaidi na anahitaji kulazwa. Hivyo akalazwa wodi ya Daraja la Kwanza.”

Aidha, Dk. Saigodi alisema licha ya uchunguzi kubaini kuwa ana tatizo kubwa zaidi, pia waligundua kuwa mapigo ya moyo yalikuwa juu ya kiwango cha kawaida.

Alisema kutokana na hali hiyo, jana asubuhi, mbunge huyo kutoka mkoani Kilimanjaro, ilibidi asafirishwe kwa gari la wagonjwa la Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kupelekwa Muhimbili.

Alisema msafara huo uliondoka jana saa 12 asubuhi ukiwa na wauguzi kadhaa wa hospitali hiyo ili kupelekwa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.

Dk. Saigodi alisema uchunguzi huo utahusisha kuangalia athari za kiharusi hicho pamoja na tatizo kubwa wanaloliona ikiwamo uchunguzi wa kichwa chake.

Kimaro aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2005 na katika siku za karibuni, amekuwa akisikika kuwa miongoni mwa baadhi ya wabunge wa CCM wanaopamba na ufisadi.

Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustino Mrema, aliyetangaza nia ya kuwania Jimbo la Vunjo katika Uchaguzi Mkuu ujao, alimpa pole na kumwombea apate nafuu ya haraka mbunge huyo.

Lakini aliongeza kuwa “mimi wakati nikienda kutibiwa India, Kimaro aliwakusanya watu Vunjo na kueleza kwamba sitarudi, napenda ajue kuwa kila mtu ni mgonjwa mtarajiwa …namwombea apone tupambane Vunjo.”

No comments:

Post a Comment