Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Monday, April 12, 2010

Nakaaya Sumari ajiunga Chadema


Mwanamuziki maarufu wa miondoko ya muziki wa kizazi kipya ‘Bongo Fleva’ Nakaaya Sumari ametangaza rasmi kujiunga na siasa katika kambi ya upinzani kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na tayari amekabidhiwa kadi namba 0227706 ya chama hicho.

Akizungumza jijini Arusha leo, Nakaaya alisema hakusukumwa wala kushawishiwa na mtu yeyote kujiunga na masuala ya siasa hususani za kambi ya upinzani bali aliamua mwenyewe kuchukua hatua hiyo muhimu ili kuleta mabadiliko ndani ya jamii ya Watanzania.

Nakaaya ambaye alivuma na kibao chake cha ni ‘Mr Politician’ kilichokuwa kikizungumzia zaidi mambo ya Siasa ambayo hufanywa na baadhi ya wagombea ambao huomba kura kwa kubembeleza lakini baada ya kupata hushindwa kufikisha kusudi na matatizo yanayowakabili wananchi katika sehemu husika badala yake hulenga zaidi maslahi binafsi.

Alisema sababu zilizomsukuma kujiunga na CHADEMA ni pamoja aina ya maisha ya ambayo Watanzania wengi wamekuwa wakiishi bila kujua hatima ya maisha yao kwa kukosa huduma nyingi muhimu. Alisema katika mazingira kama hayo Serikali imekuwa ikiingiza fedha nyingi hususani katika Sekta za Afya lakini miaka nenda rudi bado akina mama na wajawazito wameendelea kufariki dunia kwa kujifungua bila kuwa na vifaa muhimu huku wengine wakilala katika kitanda kimoja wanawake sita au wane katika wodi za wazazi.

“Hii ni fedheha kwetu kama Watanzania hususani akina mama, inakuwaje leo tangu Uhuru tuendelee kulala chini baada ya kujifungua ndani ya hospitali zetu, viongozi wa serikali wamekuwa wakiwadharau akina mama ndiyo tasfiri yake,” alisema Nakaaya.

Akitoa sababu nyingine alibainisha kwamba, hivi sasa shilingi ya Tanzania imeendelea kuporomoka ikilinganishwa na baadhi ya fedha za nchi nyingine ambazo tangu zipate uhuru wao zimeendelea kukumbwa na migogoro ya vita vya wenyewe kwa wenyewe lakini bado fedha zao zimeendelea kuimarika zaidi kuliko shilingi ya Tanzania.

“Hii ilikuwa ni ndoto yangu ya muda mrefu lakini pia nimekuwa nikikerwa na umasikini wa Watanzania wenzangu ilhali bado tumejaliwa kuwa na rasilimali nyingi kuliko hata za nchi zinazotuzunguka,” alisema Nakaaya mbele ya viongozi wa CHADEMA Mkoa wa Arusha.

2 comments:

  1. Mm kama mimi nampongeza sana Sister kwa uamuzi mzuri alio uchukua kwa sababu chadema ni chama makini kitakacho weza kuwaondoa watanzania kwenye umaskini tulio nao ambao unaletwa na chama kichokua madarakani.lazima vijana wote wapenda maendeleo tufanye alichofanya nakaya bg up sister.

    ReplyDelete