Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Sunday, March 28, 2010

Ajali nyingine kama ya Kibamba yaua 2 Mbezi

SIKU moja baada ya ajali mbaya iliyohusisha lori lililolalia Hiace na kuua watu 11 katika eneo la Kibamba Darajani, wilayani Kinondoni, ajali nyingine imetokea juzi usiku katika eneo la Mbezi Mwisho ambapo lori liliacha njia na kugonga daladala na kisha kukanyaga watu wawili waliokufa papo hapo.

Watu wengine wanane walijeruhiwa vibaya wakiwemo abiria waliokuwa wakisubiri usafiri kuelekea Kibamba waliokuwa wamesimama pembeni mwa barabara, abiria waliokuwa wakishuka katika daladala iliyogongwa, waendesha pikipiki na wafanyabiashara ndogondogo waliokuwa pembezoni mwa barabara hiyo ya Morogoro, eneo la Mbezi Mwisho. Miongoni mwa watu waliojeruhiwa ni Neema Makundi, Mkazi wa Mbezi.

Mashuhuda wa ajali hiyo waliliambia gazeti hili katika eneo la tukio juzi usiku kuwa, dereva wa Lori aina ya Scania likiwa na trela lake ambalo lilikuwa likitokea Kibaha kwenda Ubungo, lilionekana kushindwa kushika breki kama umbali wa meta 20 hivi na kuacha njia.

“Wakati alipokuwa akijaribu kukwepa daladala iliyokuwa imejaa abiria hapa, alilivaa daladala hili lililokuwa linashusha abiria na hapa palikuwa na abiria wakisubiri usafiri, mwanamume mmoja na mwanamke mmoja wamekanyagwa vibaya na kufa papo hapo, ila wengine wamejeruhiwa na kuvunjika baadhi ya viungo vya mwili,” alisema Ali Abdu (Mboma).

Ajali hiyo ilitokea saa 3.30 usiku, na gazeti hili lilishuhudia mwanamke ambaye hakufahamika jina mara moja, akiondolewa chini ya lori hilo huku akilia na nguo zikiwa zimechanika na miguu yote miwili ikiwa imevunjika. Wasamaria walikodi teksi na kumkimbiza Hospitali ya Tumbi, Kibaha.

Makundi ambaye alisaidiwa na watu kutoka katikati ya watu waliokuwa wameangukia bondeni baada ya tafrani ya kila mmoja kujinusuru na ajali hiyo, huku akilia alisema kuwa haelewi kilichotokea kwani wakati anashuka kutoka katika daladala hiyo inayofanya safari kati ya Mbezi na Kariakoo, alisikia kishindo na kujikuta chini huku akiangukia bondeni.

Wafanyabiashara walionusurika na ambao hupanga bidhaa zao pembezoni kabisa mwa barabara kinyume cha sheria, waliamua kuchukua tochi na kuanza kutafuta mikoba yao ya pesa iliyopotea bila kujali wenzao waliokufa na kujeruhiwa vibaya.

Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Charles Kenyela, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa katika ajali hiyo, mtu mmoja alikufa, abiria saba waliokuwa wakisubiri usafiri walijeruhiwa vibaya huku mmoja akiwa mahututi.

Alisema daladala hiyo ilikuwa ikiendeshwa na Roggers Manka (35) mkazi wa Mbezi ambaye alieleza kuwa alikuwa akielekea Kiluvya ingawa basi lake liliandikwa Mbezi-Kariakoo.

Kenyela alisema maiti yupo Tumbi na majeruhi pia wamelazwa huko pia. Aliwataja waliojeruhiwa vibaya kuwa ni Agnes Semkwabi, mkazi wa Tandale, Jackline John (27) na Robert Mafuru wakazi wa Mbezi kwa Yusuf, Hamis Omari (22) mkazi wa Kiluvya, Angela Fredy (21) mkazi wa Msasani, Fua Ramadhani (23) mkazi wa Msasani na mwanamume anayekadiriwa kuwa na miaka kati ya 35 na 40 ambaye jina lake halikupatikana mara moja.

No comments:

Post a Comment