Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Sunday, March 28, 2010

Polisi mbaroni kwa na dawa za kulevya

WAKATI Serikali kupitia vyombo vya Dola ikipambana na dawa za kulevya nchini na kutangaza kila mara watu inaowakamata kwa tuhuma za kuhusika na dawa hizo, polisi mwenye cheo cha Konstebo wa Dar es Salaam, ambaye anapaswa kuwa miongoni mwa wanaopiga vita biashara hiyo, amekamatwa na polisi wenziwe kwa msaada wa mgambo, akituhumiwa kuwa na shehena kubwa ya dawa za kulevya.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili juzi, zilibainisha kuwa askari huyo (jina na namba yake tunavyo), anayedaiwa pia kuwa mzoefu katika kushirikiana na majambazi na wauza dawa za kulevya, alikamatwa akiwa na dawa hizo ndani ya gari yake baada ya kufukuzwa na polisi wenzake kwa umbali wa zaidi ya kilometa saba.

Mtoa taarifa wetu alisema askari huyo anayefanya kazi katika Kituo cha Polisi Magomeni, Kitengo cha Upelelezi, alikamatwa juzi saa 10 jioni katika eneo la Kibamba, gari lake likiwa limebeba magunia nane ya mirungi na kwa sasa anashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay.

“Hivi tunavyoongea anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay, alikamatwa na Kikosi cha Doria Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, alikuwa peke yake kwenye gari na dawa hizo za kulevya,” alisema mtoa taarifa wetu.

Kaimu Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Charles Kenyela aliithibitishia HabariLeo Jumapili kuwa askari Polisi huyo amekamatwa akiwa na raia mmoja na wote wanashikiliwa na Polisi.

Kenyela akielezea namna ilivyokuwa ngumu kumkamata polisi mwenzao huyo, alisema, “ni kweli alikuwa na raia mmoja, wamekamatwa na mirungi iliyokutwa kwenye buti garini mwake, iliteremshwa katika basi la abiria la Meridian linalofanya safari zake mikoa ya Kaskazini, na yeye aliipokelea Kiluvya lakini hakukamatiwa hapo.”

Kenyela alisema kulikuwa na tafrani kubwa kabla ya kukamatwa kwani baada ya kuiweka (mirungi) katika gari yake yenye namba za usajili T 287 ATL aina ya Toyota Cresta, alitaka kudhibitiwa na mgambo aliyekuwa akimhoji kitu alichobeba, lakini kwa mwendo wa kasi, alimtoka mgambo huyo jambo lililosababisha watu kupiga simu Polisi.

“Si unajua Polisi Jamii, askari wa doria walipopata taarifa, wakaanza kumfukuza, walimfukuza weee, umbali mrefu kutoka Kiluvya mpaka eneo la Msewe huko kwenye msitu wa bonde la Golani, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ndipo wakamkamatia hapo, baada ya kumshusha kwenye gari, walimtambua kuwa ni askari,” alisema Kenyela.

Alisema walipopekua gari, walikuta mirungi ikiwa katika viroba ambavyo vimefungwa kwa utaalamu wa hali ya juu na kama vingefunguliwa, vingejaa magunia tisa ya kawaida na kiroba kimoja.

Kenyela alisema bado hawajajua gharama ya mirungi hiyo na uzito wake na kwamba wanaendelea na upimaji huku raia na askari huyo wakiwa mahabusu.

Kaimu Kamanda huyo alisema watuhumiwa hao hawatatajwa majina kwa sasa kwa kuwa wamebaini kuwa wapo askari wengi zaidi wanaojihusisha na vitendo hivyo ambao upelelezi dhidi yao unaendelea kwa nia ya kuwanasa.

“Tutamshitaki kijeshi na endapo atabainika kuhusika na tukio hilo, atafikishwa mahakamani kama raia wa kawaida,” alisema Kenyela.

Naye Anna Makange, anaripoti kutoka Tanga kuwa, Polisi mkoani hapa inawashikilia vijana wawili kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 77.

Dawa hizo aina ya mirungi zilikamatwa Machi 25 mwaka huu saa 9 alasiri katika mtaa wa Kisosora, Kata ya Chumbageni wilayani Tanga.

Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Mkoa wa Tanga (RCI), Jaffar Mohamed aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Victor Juma (26) na Kombo Bure (37) wote wakazi wa Kisosora.

Alisema watuhumiwa walikuwa wakisafirisha dawa hizo kwa njia ya pikipiki yenye namba T223 AYC aina ya Toyo iliyokuwa ikitokea mjini Mombasa katika nchi jirani ya Kenya kuletwa mjini hapa.

Matukio ya usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku nchini na kuharibu idadi kubwa ya vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.

Mohamed alisema kutokana na hali hiyo, serikali itahakikisha haitoi dhamana kwa mtu yeyote atakayekutwa akijihusisha na dawa za kulevya.

No comments:

Post a Comment