Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Saturday, March 27, 2010

Wanasiasa wampinga Shekhe Yahya


VIONGOZI wa vyama vya siasa nchini wameupuuza utabiri wa Mnajimu maarufu Afrika Mashariki, Shehe Yahya Hussein na kuitaka Serikali izipuuze ndoto hizo kwa kuhofia uchochezi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili jana Dar es Salaam, baadhi ya viongozi wa vyama hivyo walikataa kutoa maoni yao kuhusu utabiri huo, ambao Shehe huyo alitabiri kutokuwapo kwa uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema hawezi kuzungumzia masuala yanayohusu unajimu kwa kuwa hayaamini na kwamba anachokiamini ni Katiba ya nchi na ratiba ya uchaguzi.

“Sina cha kusema juu ya mambo ya unajimu, ila naomba pia waulizwe wanajimu wengine na wapiga ramli, ili kujua na wao wana msimamo gani katika hili, ila kwa kweli mimi naiamini zaidi Katiba na ratiba niliyonayo ya uchaguzi,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema pamoja na hayo, ameshangazwa na ratiba ya uchaguzi ambayo inaonesha kuwa uchaguzi mkuu utafanyika Oktoba mwaka huu badala ya Desemba, kwa kuwa uchaguzi wa 2005 ulifanyika Desemba.

“Kwa mujibu wa Katiba Rais lazima akae madarakani kwa miaka mitano na ataapishwa mwingine kipindi kilekile alichoapishwa Rais aliyepita.”

Naye Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP) Augustine Mrema, aliitaka Serikali isiupe nafasi utabiri huo, kwa kuwa una mwelekeo wa uchochezi na utaifanya nchi ionekane kama inaongozwa kwa utabiri.

“Mimi nasema Shehe Yahya asipewe nafasi na Serikali, kwani yenyewe haipaswi kuingia kwenye masuala ya imani, nchi hii ina waumini safi wa dini za Kiislamu na Kikristo, kwa hili asisikilizwe ili kuondokana na uchochezi wa ghasia,” alisema Mrema.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema kwa mujibu wa Katiba kila Mtanzania ana haki ya kuamini na kuabudu. “Serikali haina dini, lakini wananchi wana dini zao, SheheYahya ametumia nafasi ya Katiba kuzungumza anachoamini yeye, kwa hilo sina la kusema.”

Naye Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo, alisema hawezi kujiingiza katika mambo ya unajimu, hivyo asingependa hata kuuzungumzia.

Juzi alipozungumza na waandishi wa habari, Mnajimu huyo alitabiri kuwa kutokana na viashiria alivyoviona katika mwaka wa kinyota ulioanzia Machi 21 mwaka huu, hakutakuwa na uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.

Pia alikaririwa katika mkutano huo akisema: “Ninawahakikishia na kuwafahamisha kwamba mimi ninapotoa utabiri wangu huwa simlengi mtu wala simtabirii mtu, natoa utabiri kwa manufaa ya jamii, kwa hiyo ni wajibu wa kila mtu ama kukubali au kukataa haya ninayoyasema.”

No comments:

Post a Comment