Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Saturday, March 27, 2010


Bw.Freeman Mbowe.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza vita dhidi ya Mbunge wa Jimbo la Mtera, John Malecela na wabunge wenzake waliokaa bungeni kwa muda mrefu.

Vita hiyo ilitangazwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe katika mkutano wake wa Oparesheni Sangara uliofanyika wilayani Mpwapwa juzi.

Mbowe alisema kwa sasa umri wa Malecela kuendelea kuwa mbunge umekwisha na kwamba akisikia amechukua tena fomu kutetea nafasi hiyo mwaka huu atarusha helikopta katika kata zote za Jimbo hilo kuhakikisha anamng’oa.

“Mimi nazaliwa Malecela namsikia akiwa bungeni, nimesoma elimu ya msingi hadi sekondari, nimefanya kazi BoT, nimeacha kazi na sasa nafanya biashara, nimeingia kwenye siasa nimekwenda bungeni nimemkuta na nimemuacha, hivi huyu mtu amekuwa Sultani?,”alihoji Mbowe.

Alisema uwepo wa viongozi hao aliowaita masultani ndio unakokwamisha demokrasia nchini kwa kuwa hali hiyo ndiyo inayowajengea hofu wakazi wa Mkoa wa Dodoma.

Mbowe aliwataja wabunge wengine wa Mkoa wa Dodoma anaokamia kupambana nao mwaka huu kuwa ni Mbunge wa Mpwapwa, George Lubeleje na Mbunge wa Jimbo la Bahi, William Kusilla.

Mbowe ambaye alisafiri jana kwenda Muleba kuhudhuria maziko ya Balozi Christopher Ngaiza ambaye ni alikuwa kada wa chama chake, alitoa wito kwa wakazi wa Mpwapwa na vitongoji vyake kuacha ushabiki wa vyama badala yake wachague viongozi bora na wenye sifa ya kuongoza.

Kwa mujibu wa Mbowe, utamaduni wa kushabikia vyama umepitwa na wakati kwani vyama vimeundwa na binadamu tofauti na ardhi na watu wake ambao wameumbwa na Mungu.

Kuhusu kukithiri kwa umasikini, Mbowe alisema kumetokana na mfumo wa mbovu wa serikali inayoundwa na CCM.

Alisema mfumo huo umekumbatia mafisadi na kuchana dhana ya mwaasisi wa taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere aliyesema chama hicho ni cha wakulima na wafanyakazi.

Alisema Tanzania haina sababu ya kuwa maskini kwa kuwa ina kila aina ya rasilimali ikiwmao madini, mbuga za wanyama na ardhi yenye ruruba.

Kuhusu elimu alisema kuwa ujenzi wa madarasa katika kila kata umechangia kudidimiza elimu hapa nchini kufuatia shule hizo kuwa na upungufu mkubwa wa walimu na vitendea kazi.

Hata hivyo, Mbowe aliwashambulia baadhi ya wabunge wa CCM waliokuwa wakijinadi kuwa ni makamanda wa kupambana na ufisadi kuwa wameonyesha kutokuwa na uwezo wa kupambana na ufisadi.

“Hoja ya mapambano dhidi ya ufisadi iliasisiwa na Chadema, nyinyi ni mashahidi namna wabunge wa Chadema walivyopambana , mara wakajitokeza wenzetu kutoka CCM, kina John Malecela na wenzake na kujinadi ni wapambanaji wa ufisadi, lakini tulijua ngoma hii hawaiwezi na kwamba wangeishia njiani,”alisema.

No comments:

Post a Comment