Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Thursday, March 18, 2010

Tanzania kukaa giza kwa saa 5 kila siku


BAADA ya katikakatika ya umeme bila utaratibu kwa siku kadhaa, hatimaye Shirika la Umeme (Tanesco) limetangaza rasmi mgawo kwa mikoa yote Tanzania Bara kuanzia saa 12 jioni hadi saa nne usiku kila siku.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Stephen Mabada, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, alisema sababu ya hatua hiyo ni kuharibika kwa baadhi ya mitambo katika vituo vya kuzalishia umeme.

Mitambo iliyotajwa kuharibika iko katika vituo vya kuzalisha umeme vya Kidatu, Kihansi, Pangani na cha gesi cha Ubungo.

Hata hivyo, taarifa hiyo haikueleza kiasi cha megawati zitakazokosekana baada ya mitambo hiyo kuharibika.

Badala yake taarifa hiyo ilisisitiza kuwa kuharibika kwa mitambo hiyo kumesababisha upungufu wa nishati hiyo kwenye Gridi ya Taifa, hali inayolilazimu shirika kuanzisha mgawo mikoa yote.

“Athari za upungufu huo zimelilazimu shirika kuanza mgawo wa umeme kwa maeneo mbalimbali wakati wa matumizi makubwa ya umeme kuanzia saa 12 jioni hadi saa nne usiku,” ilisema taarifa hiyo. Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Badra Masoud, alipoulizwa kiasi cha megawati kitakachokosekana kwenye Gridi, alisema hawezi kuitaja kwa vile shirika bado linafanya jitihada za kurejesha baadhi ya megawati kwa kutengeneza mitambo hiyo haraka.

“Siwezi kukutajia kiasi kitakachokosekana maana naweza kukutajia idadi ya megawati, mafundi walioko kwenye mitambo wakarejesha baadhi ya megawati … hilo kwa leo siwezi kukutajia,” alisema Masoud.

Wastani wa megawati zinazotumika nchini ni takribani 700 kwa siku. Kwenye taarifa ya Mabada, kuna ahadi ya Tanesco kufanya haraka matengenezo ya mitambo iliyoharibika, ili kuondoa adha ya mgawo huo, lakini taarifa hiyo haielezi idadi ya siku za matengenezo.

Masoud alipotakiwa kueleza huo mgawo utadumu hadi lini, alisema mafundi ndio kwanza wako kwenye vituo na hawajajua ukubwa wa tatizo.

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi kama mashine hizo ziliharibika kwa siku moja katika vituo hivyo, alijibu kuwa uhabirifu huo umetokea kwa nyakati tofauti na ndiyo maana kukawa na kukatika kwa umeme mara kwa mara.

Awali Tanesco ilipoulizwa juu ya matukio ya kukatika ovyo kwa umeme hususan jioni, ilijitetea kuwa inatokana na njia kuzidiwa mzigo kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watumiaji.

Hata hivyo, jana Masoud alikiri kuwa mgawo ulishaanza wiki kadhaa zilizopita na walisita kutangaza kwa kuamini kuwa matengenezo hayo yangechukua siku chache.

“Lakini baada ya kuona ripoti za kuharibika mashine zinatokea kwenye vituo vingine, tumeona tuutarifu umma juu ya kuwapo kwa mgawo,” alisema Masoud.

Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alipoulizwa lini mgawo huo utamalizika, alisema hajui ila akasisitiza kuwa mafundi wako kwenye maeneo ya kazi usiku na mchana kuhakikisha hali inatengemaa.

“Tutahakikisha mitambo hiyo inapona haraka, maana ni suala la dharura na siwezi kutabiri lini watamaliza matengenezo,” alisema Ngeleja. Katika siku za karibuni yamekuwapo matukio ya kukatika umeme na Tanesco kuomba radhi huku wakati mwingine yakitokea nchi nzima.

Masoud katika taarifa yake ya kuomba radhi alieleza kuwa umeme huo ulikatika kutokana na hitilafu katika mashine za mtambo wa kuzalisha umeme wa gesi wa Songas katika kituo cha Ubungo.

“Tatizo hilo lilifanya mitambo mingine katika mfumo wa Gridi hiyo ya Taifa kuelemewa na mzigo, hali iliyosababisha mitambo hiyo nayo kupata hitilafu na umeme kukatika,” alisema katika taarifa yake wiki iliyopita.

Alisema juhudi zilifanyika mara baada ya tatizo hilo kutokea na shirika kufanikiwa kuurejesha umeme huo katika hali ya kawaida, ingawa kulikuwa na baadhi ya maeneo yaliyochelewa kupata umeme kutokana na matatizo madogo yaliyotokea, hali ambayo pia imeshughulikiwa.

Lakini jana Masoud alikiri kwamba kuharibika kwa mashine kwenye vituo hivyo, ndio chanzo cha kukatika umeme, jambo ambalo jana aliliweka wazi kuwa ulikuwa ni mgawo ambao ulishaanza.

Hali hii inadhihirisha kauli aliyowahi kuitumia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kuwa “ombhisabhisa obhurweri kiriro kirimbura (mficha maradhi kilio humuumbua)”.
CHANZO HABARI LEO

No comments:

Post a Comment