Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Saturday, March 27, 2010

Stars, Somalia vitani leo!!!


Kocha Wa Taifa Stars Marcio Maximo.

TIMU ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, leo inashuka katika Uwanja wa Uhuru kuwakaribisha Somalia katika mechi ya kampeni ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Afrika kwa nyota wa ligi za ndani-CHAN-zitakazopigwa mwakani nchini Sudan.

Ingawa mechi mbili baina yao ndizo zingeamua timu ya kusonga mbele, lakini kutokana na machafuko ya kisiasa nchini Somali, mechi ya leo ndiyo itaamua.

Akizungumzia mechi hiyo, Kocha Mkuu wa Stars, Marcio Maximo, alisema licha ya ubora wa wapinzani wao, vijana wake wamejipanga vizuri kushinda mechi.

Maximo alisema, ni muhimu kushinda mechi hiyo ya pekee na hasa ikizingatiwa kuwa Stars inacheza nyumbani ili kujiweka katika nafasi na mazingira ya kufanya vizuri katika mechi zitakazofuata.

“Kama ukianza vizuri katika mechi za mwanzo inakupa nguvu ya kufanya vizuri zaidi katika mechi nyingine, hivyo nina matumaini timu yangu itashinda mechi yetu hiyo iliyojaa ushindani mkubwa,” alisema Maximo.

Maximo amewasihi wapenzi, mashabiki na Watanzania kwa ujumla, kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu hiyo ili kuwapa wachezaji ari na nguvu ya kufanya vizuri.

Kwa upande mwingine, wadhamini wa Stars kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), jana ilikabidhi timu hiyo hundi ya sh milioni 50 ili kuwaongezea wachezaji hamasa.

Mshindi wa leo atacheza na Rwanda.

Akipokea hundi hiyo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Frederick Mwakalebela, aliishukuru SBL kwa kuisaidia timu hiyo na kuomba makampuni na wadau wengine wazisaidie timu za taifa.

Mwakalebela alisema maandalizi ya mechi hiyo yamekamilika na tiketi za mchezo huo zitaanza kuuzwa leo kuanzia saa tatu asubuhi.

Viingilio vitakuwa shilingi 30,000 kwa viti maalu; 15,000 Jukwaa Kuu; 10,000 Jukwaa la kijani; na 3,000 mzunguko.

Somalia iliwasili juzi tayari kwa mchezo wa leo huku kocha wake Mohamed Abdulahi na nahodha wa timu hiyo, Yusuf Ali Nur, wametamba kuibuka na ushindi licha ya kukiri kuwa Stars ni wazuri.

No comments:

Post a Comment