Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Friday, March 26, 2010

MREMA AMPELEKA SITA KORTINI!


MH Augustino mrema.

MWENYEKITI wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) Augustine Mrema, amemfungulia rasmi kesi ya madai Spika wa Bunge, Samuel Sitta na kumtaka amlipe fidia ya Sh bilioni moja kwa kumkashifu na kumdhalilisha kwa makusudi.

Mrema alisema jana Dar es Salaam kuwa kesi hiyo namba 32, aliifungua katika Mahakama Kuu ya Tanzania na bado haijapangiwa Jaji wa kuisikiliza wala tarehe ambapo pamoja na Spika, pia Mhariri wa Mwananchi na kampuni ya Mwananchi Communications nao wamejumuishwa.

“Nimeamua kufanya hivi ili nirudishe heshima yangu ambayo nimeifanyia kazi kwa miaka 10 nikiwa waziri na kiongozi serikalini, lakini sasa nimetukanwa na kushushiwa hadhi kuwa eti ‘nimefulia’,” alisema Mrema.

Alisema Sitta katika gazeti la Mwananchi toleo namba 03548 la Machi 5 mwaka huu, alikaririwa akimwelezea Mwenyekiti huyo kuwa amekwisha kisiasa na kifedha na sasa anahangaika kujinasua katika hali hiyo.

“Katika gazeti hilo, Spika Sitta amediriki hata kunituhumu kuwa napata fedha ili kuipigia debe CCM, hali ambayo inaashiria kuwa nakula rushwa … siku hizi nikisikia hodi mlangoni napatwa na hofu nikifikiri ni polisi wanakuja kunikamata, maana Sitta ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM amesema nakula rushwa,” alisema.

Alisema kauli hiyo ya Spika kwa mujibu wa gazeti hilo, aliitoa alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu madai ya Mrema kwenye mkutano wake na waandishi wa habari Machi 4 mwaka huu, kuwa Sitta amekiuka maadili ya uongozi akiwa Spika wa Bunge, kwa kuendeleza mjadala wa kashfa ya Richmond na kushiriki ziara na baadhi ya wabunge wanaojipambanua kuwa ni wapambanaji wa ufisadi.

Akizungumzia madai hayo gazeti hilo lilimkariri Sitta akisema, “Mrema ni mhuni na amepitwa na wakati … pia amefilisika kisiasa na kifedha, sasa anatafuta njia ya kujinasua kutoka hali hiyo,” Mrema alilikariri gazeti hilo.

Mrema alisema kauli ya Sitta imemchafua mbele ya Watanzania ambao sasa wanamwona ‘amefulia’ na kwa watu ambao walikuwa wanamwamini na kumheshimu, sasa wamepoteza imani naye.

“Yaani mimi ‘nimefulia’ mnajua maana ya kufulia, ni mtu aliyekosa hata hela ya kula, mimi Mrema ninaongoza TLP ambayo katika uchaguzi wa serikali za mitaa imeshika nafasi ya nne kati ya vyama 18 vilivyopo, sasa nimefilisika vipi kisiasa, hii ni kashfa na matusi,” alisema.

Alisema Spika ni kiongozi wa chombo muhimu kinachowakilisha wananchi na kauli aliyoitoa kuhusu Sitta kuwa amekiuka maadili, ni ushauri, kwa kuwa akiwa kiongozi wa chombo hicho, hapaswi kuwa na makundi au kuegemea upande, hali ambayo itakuwa ni vigumu kwake kutoa uamuzi wa haki.

“Nimeifungua kesi hii kwa kuwa hata baada ya gazeti la Mwananchi kutoa taarifa hiyo, nilimwandikia barua ya kuniomba radhi na kunipa fedha ya kifuta jasho lakini amenidharau, kibaya zaidi kwa kauli yake hiyo, muda wowote naweza kukamatwa, sasa nataka anilipe Sh bilioni moja; yeye ni Spika hiyo ni fedha kidogo kwake,” alisema.

Alisema amehuzunishwa na kauli ya Spika kuwa amekuwa akiipigia debe CCM. “Kwa uwezo gani nilionao mimi Mrema na kwa nini anisingizie, CCM imeshinda uchaguzi tangu mwaka 2000 na 2005 bila msaada wangu.”

Mrema alisema anachojua yeye ni kwamba Spika Sitta anafahamu anataka kugombea jimbo la Vunjo, hivyo ili kumsaidia rafiki yake ambaye ndiye mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Aloyce Kimaro, aliamua kumchafua.

Alisema kwa kashfa ya ‘kufulia’ si kweli na ushahidi anao, kwani kwa mujibu wa taarifa ya akaunti yake katika benki ya NMB, ana akiba ya Sh milioni 37. “Mimi ni milionea, kuliko hata Waziri Mkuu wangu Mizengo Pinda ambaye ana Sh milioni 25 benki,” alisema Mrema.

Sitta naye alikaririwa kutaka kumfungulia kesi ya madai Mrema na kumtaka athibitishe matamshi yake ya kwamba alishirikiana na wabunge wanaojipambanua kama makamanda wa vita dhidi ya ufisadi na wafadhili wao kufanya ziara mikoani.
chanzo habari leo!

No comments:

Post a Comment