Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Friday, March 26, 2010

Breki chanzo cha ajali ya Kibamba

UKOSEFU wa breki umeelezwa kuwa ndicho chanzo cha ajali ya lori na daladala iliyosababisha vifo vya watu 11 katika eneo la Kibamba, nje kidogo ya Dar es Salaam jana.

Hadi jana maiti watano kati ya 11 waliokufa katika ajali hiyo, walikuwa wametambuliwa akiwamo mjamzito na kondakta wa daladala. HabariLeo ilishuhudia kazi ya uopoaji maiti katika ajali hiyo iliyohusisha daladala Toyota Hiace namba T 615 AJW ikitoka Kibamba kwenda Ubungo na lori la mafuta aina ya IVECO Fiat namba T 189 ABP na tela lake namba T192 ABP.

Abiria wote wa daladala walikufa papo hapo baada ya kugongwa na lori hilo na kutumbukia mtaroni na kulaliwa.

Lori inadaiwa lilikuwa na shehena ya lita 30,000 za mafuta ya taa. Lori hilo linalomilikiwa na Mohamed Mahmoud lilikuwa likiendeshwa na Kudra Adam (30) ambaye alikimbia baada ya ajali.

Hiace inamilikiwa na Seleman Khalfan Rajab. Mamia ya wakazi wa Kibaha walifika eneo la tukio kwa ajili ya kutambua ndugu zao huku baadhi wakidai kuwa ajali hiyo ilitokea saa 11 alfajiri kulingana na muda ambao ndugu zao waliondoka majumbani kuwahi shughuli zao.

Miongoni mwa waliotambuliwa ni Shukuru Hussein (27) aliyetambuliwa na baba yake mzazi, Hussein Saleh, ambaye alisema mwanawe alikuwa kondakta wa daladala lingine, na alikuwa anawahi kufuata gari lake Mbezi.

Mwingine ni Faraj Ismail Ngalamba aliyekuwa kondakta wa daladala lililopata ajali ambaye alitambuliwa na kaka yake, aliyedai kuwa asubuhi ile alimpigia simu lakini hakumpata.

Maiti mwingine aliyetambuliwa ni Abdultwaibu Twalib aliyetambuliwa na mkewe, Shani Mustafa ambaye alidai kuwa mumewe alikuwa akiwahi kazini bandarini Dar es Salaam.

Aliyetambuliwa mwingine ni Ester Paulo, aliyekuwa mjamzito na alitambuliwa na ndugu zake baada ya mwili wake kuvutwa huku tumbo likiwa limepasuka; na Zainabu Ali. Maiti wote wanasadikiwa kuwa wa Kibamba kutokana na daladala hilo kuanzia safari yake Kibamba njia panda.

Hata hivyo, kazi ya uopoaji ilionekana kuwa ngumu na kuchukua zaidi ya saa sita tangu ajali itokee kutokana na askari Polisi na kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, kufika eneo la tukio lakini bila vifaa madhubuti vya kuopolea miili hiyo.

Sambamba na uopoaji maiti, wananchi wengine mawazo yao yalielekea katika jinsi ya kujichukulia mafuta ya taa huku wakionekana na ndoo kwa ajili hiyo. Baada ya saa tano kupita, lilipofika gari la kuvuta magari mabovu aina ya Effco Crane kutoka kampuni ya BMK lililokodiwa kutoka Oysterbay likijikongoja polepole na baada ya kufika, lilisababisha barabara ya Morogoro kufungwa kwa zaidi ya saa mbili kupisha kazi ya kutenganisha magari hayo.

Tukio hilo lilivuta watu wengi wakiwamo wasafiri waliokuwa wakipita eneo hilo, ambapo kijana aliyejulikana kwa jina la Sijali alijikuta akiangua kilio kilichowashtua mashuhuda hao, baada ya kumtambua mama yake kupitia kiatu chake.

Askari walimsaidia kumpeleka katika gari lenye miili ili kumtambua mama yake zaidi, na alikiri kuwa ni yeye na kuendelea kulia. Inadaiwa mama huyo hakuwa na muda mrefu tangu ahamie Kibamba.

Baada ya kazi hiyo, maiti wawili waliotolewa mapema walipelekwa katika hospitali ya Tumbi, Kibaha na wengine hospitali za Mwananyamala na Muhimbili.

Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga, alithibitisha kuwa lori lilikuwa na lita 30,000 za mafuta ya taa na inadaiwa lilikosa breki na kulipamia daladala na kuliburuza meta kadhaa mtaroni na kulilalia.

Alisema maiti wanane waliopolewa na vipande vya mikono na viwiliwili ingawa inawezekana kuwapo zaidi, lakini hakuna aliyenusurika. Hata hivyo, alisema ipo haja ya barabara ya Morogoro hasa eneo hilo kufanyiwa marekebisho, kutokana na kuwa tishio kwa ajali.

Alikiri kuwa tatizo kubwa linalolikabili Jeshi la Polisi ni kukosa vifaa vya uokoaji kutokana na kwamba tangu walipopata taarifa, yalifika magari matatu ya kuvuta magari mabovu lakini yote yalikuwa hayana uwezo wa kulivuta lori hilo.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk. Mutani Suleiman, alisema alipokea maiti watano kati ya tisa ambapo wanne walipelekwa Muhimbili.

Wakati huo huo, kwa niaba ya uongozi wa Chadema mkoa wa Kinondoni Kanda Maalumu ya Dar es Salaam; Mwenyekiti wa Chama hicho katika kanda hiyo, John Mnyika, ametuma salamu za rambirambi kwa ndugu, jamaa na marafiki wa wafiwa wa ajali hiyo.

Pia ametoa mwito kwa Serikali na vyombo vya Dola, kufanya uchunguzi wa kina kuhusu vyanzo vya ajali za mara kwa mara katika eneo la Kibamba, ambazo zimekuwa zikisababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.

“Ikumbukwe, kuwa Desemba 2007 ajali nyingine ilitokea Kibamba Hospitali, ikihusisha malori na kusababisha vifo vya watu saba akiwamo mjamzito na wengine 11 kujeruhiwa,” alisema Mnyika.

Aprili mwaka juzi, alisema jumla ya watu 181 walipoteza maisha kwa kugongwa na magari kati ya mwaka 2005 hadi mwaka 2007 katika eneo kuanzia Kibamba hadi Ubungo kwenye mataa.

“Mei mwaka jana, madereva wawili walikufa baada ya magari yao kugongana uso kwa uso maeneo hayo ya Kibamba … Januari mwaka huu, watu 18 walijeruhiwa katika ajali ya gari Kibamba Darajani ambapo magari matano yaligongana kwa wakati mmoja,” alisema.
chanzo habari leo

No comments:

Post a Comment