Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Sunday, March 7, 2010

AJALI ZAWA KERO SASA KHAAA JAMANI!

basi lililogonga treni


gari hili lililonga scania ya mafutaGari lililovamia muembe
Habari za leo Ankal,
Katika siku za hivi karibuni nimekuwa nikiogopa kuangalia taarifa za habari na wanangu kwa kujua kwamba habari ya kwanza itakua inahusu ajali na zitaonyeshwa picha za maiti na majeruhi. Kwa hesabu za haraka haraka, nafikiri idadi ya watu waliofariki kwa ajali za magari mwaka huu hapa nchini hazipishani sana na idadi ya watu waliofariki dunia kwa tetemeko la ardhi huko Chile.

Kinachonistua mimi zaidi ni Serikali yetu kutoonekana kuwa na mkakati mzuri wa kupunguza au kuondokana kabisa na ajali hizi. Kwa muda huo wote nilikuwa najaribu kutafuta suluhisho la majanga haya kwa kuwa najua katika kila ajali kuna familia zinapoteza mzazi, mkuu wa familia au mtoto na Watanzania kwa ujumla tunapoteza nguvu kazi muhimu. Katika ajali hizo pia kuna wanaopata majeraha makubwa na kupoteza viungo na hivyo kupungukiwa na uwezo wa kujiendeleza kiuchumi.

Mara nyingi habari huwa ile ajali yenyewe na vifo vilivyosababishwa na ajali hiyo. Kinachotokea siku na miezi baada ya ajali hakipati nafasi tena katika vyombo vya habari. Huwa hatujiulizi, je, ajali ile ilisababishwa na makosa ya nani? Je, majeruhi wote walipona na wale waliopoteza viungo walipata msaada gani? Je, waathirika huwa wanalipwa fidia yeyote au kila mtu na lwake? Je, wamiliki wa mabasi hukata bima zinazowalinda abiria?

Maswali ni mengi lakini kwa sasa naona ni muhimu kupata ufumbuzi wa tatizo lenyewe. Katika kujaribu kutatua tatizo hili nadhani vitu kadhaa inabidi vifanyike

Leseni zote daraja C zisimamishwe matumizi yake kuanzia Julai 2010 mpaka hapo dereva husika atakapohudhuria mafunzo maalumu yatakayoratibiwa na NIT na VETA ambayo yatamfundisha dereva kuwa makini awapo barabarani, jinsi ya kutoa huduma ya kwanza, uhusiano mzuri na mteja na jinsi ya kukagua gari lake.
Wahitimu wa mafunzo hayo watapewa “smart card” ambazo zitaingizwa kwenye mtandao. Kwa kuanzia Jeshi la Polisi linaweza kushirikiana na mashirika ya NSSF na PSPF kutoa kadi hizo, kuhifadhi picha, alama za vidole pamoja na habari zote za mhusika kwenye mtandao wa kompyuta. Mashirika haya yana uwezo huo kiteknolojia na yana ofisi nchi nzima.
Kila dereva wa gari la abiria atatakiwa kuvaa kitambulisho hicho (smart card) muda wote atakaokuwa kazini.

Nakala ya kitambulisho hicho (A4) itatakiwa kuwepo nyuma ya kiti cha dereva sehemu ambayo abiria ataweza kuiona. Dereva mmoja ataruhusiwa kuendesha gari si zaidi ya masaa 11 kwa kipindi cha masaa 24.
Jeshi la polisi likishirikiana na SUMATRA lianzishe kikosi maalumu cha barabara kuu (highway patrol) ambacho kitakuwa na jukumu la kuorodhesha madereva wote watakaokuwa wanafanya kazi katika barabara hizo. Kikosi hicho kitapewa uwezo wa kutoza faini za papo kwa papo pamoja na kupunguza pointi za dereva kila atakapofanya kosa.
Kila kosa litakuwa na pointi yake na dereva akifanya makosa mengi katika kipindi cha mwaka mmoja leseni yake itasitishwa.

Kampuni za simu zisaidie kampeni kwa kutoa namba za simu motomoto (hotline) ambazo zitaandikwa kwenye bodi za mabasi kwa ajili ya wananchi kuripoti madereva watakaokiuka sheria.

Mabasi yote yatatakiwa kuwa na namba za kuyatambulisha (Vehicle Identification Number - VIN) itakayochorwa ubavuni mwa basi ili kulitambulisha basi hilo kiurahisi.

Basi litakalopata malalamiko mengi zaidi kutoka kwa wananchi litafuatiliwa kwa siri na wakaguzi maalumu kutoka SUMATRA (Highway Marshals) ili kuthibitisha madai ya wananchi.

SUMATRA iwe na kikosi maalumu cha uokozi chenye vifaa vya kisasa na mafunzo maalumu. Gharama za uokozi zaweza kufidiwa baadae na kampuni za bima.
TBS ikishirikiana na wataalamu wengine wa nje na ndani ya nchi watafute jinsi ya kupima bodi za mabasi na kuthibitisha usalama wa matumizi yake.
Inawezekana kuwa hatua hizi zikasaidia kupunguza kwa kiwango kikubwa sana ajali barabarani.
Bila shaka, zitategemea sana mabadiliko kwenye muktadha wa kuendesha shughuli za barabarani kwa wadau wote. Kupita yote, hatua hizi zitakuwa na tija pale tu ikiwa suala la rushwa barabarani litatokomezwa kabisa, na wananchi watashirikiana ipasavyo na vyombo vya usalama
mwandishi inno lyimo!

No comments:

Post a Comment