Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Saturday, March 6, 2010

Basi lingine AM Coach laua tena Tabora jana jioni

WIMBI la ajali mkoani hapa limeendelea, baada ya jana kutokea ajali ya nne mfululizo ndani ya wiki moja, kwa basi lingine la kampuni ya AM Coach kupinduka na kuua abiria mmoja na kujeruhi wengine 27 mmoja hali yake ikiwa mbaya.

Abiria aliyefariki dunia ni mwanamke anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 70 ambaye hajatambuliwa jina, lakini Msemaji wa Jeshi la Polisi, alisema jana kuwa juhudi zinafanywa kutafuta ndugu zake kupitia nyaraka alizokutwa nazo.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Tabora, Dk. Leslie Mhina, alimtaja majeruhi aliyeumia mkono wa kulia uliosagika kutokana na kukandamizwa na kitu kizito, kuwa ni Pelesi Leonard (70), na juhudi zinafanywa apelekwe Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza.

Hii ni ajali ya nne kutokea mkoani hapa kwa mwezi huu ambapo basi lingine la AM Coach liliua abiria 26 mjini Nzega; ajali nyingine mbili zikatokea Igunga na kuua mtu mmoja Jumatano wiki hii.

Miongoni mwa majeruhi wa ajali hiyo walidai chanzo cha ajali hiyo ya jana ni mwendo kasi uliochangiwa na ushindani kati ya dereva wa basi hilo na mwenzake wa kampuni ya Mohamed Trans, waliokuwa wakifukuzana kutoka stendi kuu ya mabasi mjini hapa.

Akizungumzia ajali hiyo, Pantaleo Anthony (40), ambaye ni majeruhi na mkazi wa Igunga mkoani hapa, alisema kutokana na mwendo kasi, dereva wa basi hilo alishindwa kumudu kona ndipo likapinduka.

Basi lililopinduka ni nambaT698 ATB ambalo lilikuwa likitoka Tabora kwenda Mwanza likiendeshwa na Alfred Mtandi, ambaye imeelezwa na majeruhi kuwa alitoka kupitia kioo cha mbele na kutokomea porini mara baada ya ajali.

Kwa mujibu wa Dk. Mhina, abiria waliofikishwa hospitalini hapo wakiwa majeruhi ni Cellina Palla (37) wa Cheyo, Tabora; Betty Lazaro (24) wa Kanyenye, Tabora na Tatu Jumanne (20) wa Sumbawanga, Rukwa.

Wengine ni Raphael Edward (21) wa Sikonge, Tabora; Anjelina Kasala (20) wa Nzega, Tabora; Sophia Jumanne (30) wa Mpanda Rukwa na Tabu Rajabu (31) wa Tabora.

Majeruhi wengine ni Agosti Christopher (33) wa Ipuli,Tabora; Ester Kagwe (13) wa Mpanda, Hamis Omary (35)wa Gongoni, Tabora; Rafael David (47) wa Dar es Salaam, Kape Haruna (21) wa Nzega, Idd Kabagusha(21) wa Mpanda, Bernard Mihayo (37) wa Nzega, Mpesiwa Ndamanyape (36) Kahama, Shinyanga na Kasmir Baha (33) wa Arusha.

Wengine ni Majuto Kapulilo (39) wa Tabora, Adam Gunda (30) wa Arusha, Neema Salvatory (19) wa Mpanda, Happy Kapangula (21), Mrisho Abdul (24) na Cecilia Leonard (18) wote wa Tabora; Mariam Joseph (21) wa Tinde, Mteka Kabakusha, Jackson Mhono(31) na David Raphael (11).

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Liberatus Barlow, aliwambia waandishi wa habari ofisini kwake kwamba chanzo cha ajali ni dereva kuendesha mwendo wa kasi. Alisema polisi wanaendelea kumtafuta dereva huyo.
Na kader Adara

No comments:

Post a Comment