Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Monday, March 8, 2010

Kakobe agonga mwamba


SERIKALI imelikataa ombi la Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF) la kutaka kupindisha nguzo za njia kuu ya umeme yenye msongo wa 132 kV kuepusha kile anachodai athari kwenye kituo chake cha televisheni anachotarajia kukianzisha.

Juzi Kakobe ambaye amekuwa katika mabishano na Serikali kwa takribani miezi miwili, alishauri nguzo hizo zinazopitia kando ya barabara ya Sam Nujoma zipindishwe ili zisipite karibu na kanisa lake kwa madai kuwa nyaya hizo zenye msongo mkubwa wa umeme zitakuwa na athari kwa televisheni ya kanisa hilo.


Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja akitangaza uamuzi wa Serikali jana, alisema kwamba mradi huo hauna athari mbaya kwa wananchi na mali zao na kueleza kwamba serikali imetafakari na kuona upindishaji njia hauwezekani, Ngeleja alisema Serikali inaamini kwamba Kakobe na waumini wake wataridhia sababu zilizotumika kulikataa ombi lake aliloliwasilisha juzi wakati wa kikao cha pamoja kati yake na wataalamu.

Alitaja sababu tatu kuu zilizozingatiwa kulikataa ombi lake la kupindisha njia na kuweka nguzo hizo katikati ya barabara ya Nujoma .

Alisema katikati ya barabara hiyo kumesimamishwa taa za barabarani na pia eneo hilo linakusudiwa kutumika kwa ajili ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi Dar es Salaam (DART) jambo ambalo ni vigumu kuweka nguzo za umeme.

Serikali imeona pia kwamba kanisa hilo halijawasilisha maombi kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya kuanzisha kituo hicho cha televisheni.

“Inakuwa vigumu kwa Serikali kubadili usanifu wa mradi kwa vile hatuna uhakika endapo maombi hayo ya kujenga kituo cha televisheni yatakapowasilishwa yatakidhi vigezo kwa mujibu wa TCRA ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa masafa kwa ajili ya kituo cha televisheni na teknolojia ya vyombo hivyo vya televisheni tarajiwa,” alisema Ngeleja.

Ngeleja ambaye amezisihi taasisi na mamlaka zote zinazohusika kushirikiana na Tanesco kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi kwa manufaa na ustawi wa taifa, alisema serikali itaiomba TCRA iishauri ipasavyo pindi itakapoyapokea na kukamilisha tathmini ya maombi ya Kanisa hilo la FGBF.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Stephen Mabada alisema baada ya kuwepo malalamiko ya Kanisa hilo, iliwalazimu kuwalipa wataalamu kutoka Taasisi ya Wataalamu wa Viwanda ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (BICO) Sh milioni 25 kupima na kutathmini madhara ya afya za binadamu na mitambo ya mawasiliano yatakayotokana na ujenzi wa laini hiyo.

Ingawa Ngeleja alisema Serikali haikuona haja ya kukokotoa hasara nyinginezo ikiwemo muda uliopotea wa takribani miezi miwili bila mradi huo kuendelea, kulingana na taarifa ya Tanesco, endapo mradi utaendelea kucheleweshwa hadi Machi 25 mwaka huu bila kuanza, athari zake zitakuwa kubwa.

Ucheleweshwaji wa mradi huo ambao hata hivyo serikali imesema ina matumaini Kanisa litauridhia uamuzi huu uliotolewa jana, umetajwa kwamba unaweza kuwafanya wafadhili kuifikiria serikali vinginevyo.

“Kuchelewa kutekelezwa kwa mradi huu kutasababisha gharama za mradi kuongezeka, hali ya upatikanaji wa umeme wa uhakika katika maeneo husika kuendelea kuwa mbaya na uwezekano wa wafadhili wa miradi kama hii kujitoa kusaidia katika miradi ya maendeleo,” alisema Ngeleja.

Mradi huo wa kuimarisha mifumo ya usambazaji umeme ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati mpana wa serikali. Mradi huu wa Dar es Salaam, pamoja na miradi mingine inayotekelezwa Kilimanjaro na Arusha, inafadhiliwa na taasisi mbalimbali za fedha za kimataifa.

Kwa upande wa Dar es Salaam unafadhiliwa na Benki ya Dunia pamoja na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA).

Japan inafadhili ujenzi wa njia inayolalamikiwa na Kakobe ambayo ni njia kuu ya umeme wa msongo wa kV 132 kutoka Ubungo hadi Makumbusho na kituo cha kupoza umeme eneo la Makumbusho ikipita pembezoni mwa barabara za Sam Nujoma na Ali Hassan Mwinyi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Serikali, mradi huu ni muhimu kwa kuwa utaimarisha usambazaji wa umeme kwenye maeneo ya Mikocheni, Mwenge, Kinondoni, Masaki na hivyo kupunguza mzigo mkubwa unaobebwa na vituo vingine vya kusambazia umeme kama Ilala na Ubungo.

Kukamilika kwa mradi huo kunategemewa kusaidia kupunguza kwa kiwango kikubwa kukatika kwa umeme mara kwa mara kunakosababishwa na uhaba na uchakavu wa njia za kusafirishia umeme.

“Hatushindani na Kakobe bali ni suala la hoja…hii ni nchi yetu sote. Hili suala ni la maslahi ya taifa. Nani asiyefahamu madhara ya kukatika umeme? Tunaomba Watanzania wote na waumini watoe ushirikiano.

“Mjadala haukuwa wa kupata ni nani zaidi. Hatukusudii waendelee kuweka vikwazo,” alisema Ngeleja baada ya kuulizwa njia ambazo serikali inaweza kutumia iwapo Kakobe hataridhia tamko la jana.

Hata hivyo katika kikao cha juzi, Serikali ilitatua utata juu ya vipimo na hivyo Kakobe kuridhia kwamba majadiliano yaliyobaki hayahusiani na afya kama ilivyokuwa awali. Badala yake akasema suala lipo kwenye athari kuhusu kituo tarajiwa cha televisheni.

Waumini wa Kanisa hilo linaloongozwa na Kakobe walianza kuweka kambi ya kulinda eneo lao tangu Desemba 21 mwaka jana wakizuia ujenzi wa minara ya mradi huo. Kikao cha kwanza cha kutafuta suluhu kilifanyika Januari 14 mwaka huu kabla ya cha juzi.
Na mwandishi wetu dsm!

No comments:

Post a Comment