Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Saturday, May 29, 2010

Chadema yaungana na maaskofu!


Siku moja baada ya maaskofu kuzindua umoja wao na kuiomba serikali kubadili siku ya Uchaguzi Mkuu kutoka Jumapili kwenda siku za kazi, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeunga mkono ombi hilo na kuitaka serikali kulifanyia kazi bila kusita.

Chama hicho kimesema kupanga Uchanguzi Mkuu kufanyika siku ya Jumapili inasababisha wakristo wanaotumia siku hiyo kwa ibada kukosa haki yao ya kuchagua viongiozi wao kutokana na baadhi yao kubanwa na masuala ya kiimani siku nzima na kushindwa kupiga kura.

Akikaririwa mapema jana Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe alisema suala la Uchaguzi Mkuu ni nyeti hivyo ni vizuri ikatengewa siku moja ya kazi badala ya kutumia siku ya Jumapili kama ilivyozoeleka.


“Hoja ya Maaskofu ni zuri na ina umuhimu wake, kimsingi Uchaguzi Mkuu ni suala nyeti sana na linatakiwa liwe na siku yake tofauti, badala ya kuchukuliwa kama ilivyo sasa, hata katika nchi zilizoendelea hawafanyi uchaguzi Jumapili, ni vizuri tukitenga siku moja ya kazi kuwa ni ya Uchaguzi Mkuu,” alisisitiza Bw. Mbowe.

Alisema siku za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili zinapaswa kutumiwa na viongozi wa dini na waumini wao kuombea Uchaguzi Mkuu, hivyo hazistahili kutumika kama siku za uchaguzi.

“Wapo baadhi ya watu wanakosa haki yao ya msingi ya kupiga kura kwa kuwa wanabanwa na mambo ya kiimani na haki yao kufanya hivyo, baadhi ya watu pia wanatumia siku hiyo kupumzika na hawako tayari kufanya kazi ya kujipanga kwenye mistari ya kupiga kura, siku moja ya kazi ikitumika kwa ajili ya uchaguzi Mkuu ni bora zaidi,” alisisitiza Bw. Mbowe.

Alipoulizwa kuhusu athari za kiuchumi kwa Taifa zima kupoteza siku nzima kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu badala ya kuzalisha, kiongozi huyo alisema manufaa ya uchaguzi ni makubwa kuliko siku moja ya kazi kwa kuwa watu wasipotumia siku hiyo moja vizuri athari zake ni kubwa na hudumu kwa kipindi cha miaka mitano.

Lakini Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Yusuph Makamba alipoulizwa msimamo wa chama chake kuhusu kauli hiyo, aliema kwamba yeye na chama chake ni watumishi wa bwana hivyo watafuata kile kitakachoamriwa na bwana wao (Tume ya Taifa ya Uchaguzi).

“Mimi ni mtumishi wa bwana, na bwana wangu ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), nitafanya kile atakachoagiza bwana wangu, sina cha kusema hapo nasubiri bwana wangu apange iwe ni siku gani mimi nitafuata,”alisema Bw. Makamba.

No comments:

Post a Comment