Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Monday, May 17, 2010

KitendawiliNa Musa Mateja
Zikiwa zimepita siku 44 (wiki sita na siku 2) tangu aliyekuwa mnenguaji bei mbaya nchini, Monica Vincent ‘Diana Aston Villa’ afariki dunia, kauli nzito aliyoitoa mwaka jana alipokuwa anaugua, imeanza kuibua viulizo.
Kikubwa kinachotesa ubongo ni kitendawili alichokiacha kuhusiana na majina ya mastaa ambao aliwataja kwamba anakufa lakini nao ni lazima watamfuata.

The Biggest IQ Paper, Ijumaa Wikienda lipo kwenye nafasi nzuri kutoa muongozo wa kile kinachoendelea na jinsi waliotajwa wanavyonyooshewa vidole pasipo wanyooshaji kuwa na ufahamu wa kile kilichokuwemo kwenye kifua cha Diana.


Ramadhan Masanja ‘Banza Stone’

Waliotajwa na Diana ni mafahari wa muziki wa dansi, Ally Choki ‘Mzee wa Mipango’, Ramadhan Masanja ‘Banza Stone’, Mr. Nice Lucas Mkenda, Steven Mangere ‘Steve Nyerere’ na mkongwe, Abou Semhando ‘Baba Diana’.
Wanenguaji wawili ‘big names’ ndani ya himaya ya Bongoland, Lillian Tungaraza ‘Internet’ na Aisha Mohamed Mbegu ‘Madinda’, wanatimiza orodha ya mastaa waliodaiwa na Diana kwamba akifa wao watamfuata.
Uchunguzi wa Ijumaa Wikienda umebaini kuwa kauli ya Diana kuhusu mastaa hao ni kitendawili kigumu kuteguka kwa sababu hakutoa ufafanuzi wala kueleza tafsiri ya kile alichokizungumza.


Mr. Nice Lucas Mkenda

Aidha, utata wa ugonjwa uliokuwa unamsumbua Diana ni pointi nyingine inayoibua viulizo vingi kwa sababu hakufafanua uhusiano wa maradhi aliyokuwa nayo dhidi ya mastaa aliowataja.
Utata zaidi unachukua nafasi kutokana na ukweli kwamba wote waliotajwa, ni wale ambao waliwahi kuwa watu wake wa karibu kikazi, kimapenzi na hata kirafiki.


Ally Choki ‘Mzee wa Mipango’

Mr. Nice, Steve Nyerere na Banza Stone kwa nyakati tofauti walithibitika kutoka kimapenzi na Diana enzi za uhai wake, huku mtajwa namba moja kwenye aya hii akikoleza undugu kwa kuzaa naye mtoto mmoja.
Kwa upande wa Lillian Internet na Aisha Madinda, wao walikuwa marafiki chanda kwa pete na Diana, kwahiyo kauli yake hiyo inazidi kuchanganya muktadha!

Aidha, Lillian alikuwa mwandani wa Choki, kukosekana kwa ufafanuzi wa Diana juu ya kauli yake na kutokuwepo na vielelezo vinavyoonesha uhusiano wa moja kwa moja na stadi huyo wa dansi ni pointi nyingine inayoshamirisha alama ya kuuliza!Monica Vincent ‘Diana Aston Villa’

Mbali na urafiki wa mtu na shemejiye, Diana na Choki waliwahi kufanya kazi pamoja wakiwa kwenye Bendi ya African Stars International ‘Twanga Pepeta’.
Alama kubwa ya kuuliza ipo kuhusu Baba Diana, kwa maana kile kinachojulikana ni kwamba mkongwe huyo alikuwa bosi wa Diana Twanga Pepeta, hivyo swali tata ni kwanini alitajwa?
Kutokana utata huo, gazeti hili lilizungumza na baadhi ya watajwa, hivyo kutoa ufafanuzi wao, ingawa karibu wote waliruka kwa maelezo kwamba hata wao hawajui Diana alimaanisha nini.

Akizungumza na gazeti hili wiki iliyopita, Aisha Madinda alisema kuwa suala la kufa ni la kila mtu, hivyo akadai kwamba anaamini Diana alimtaja baada ya kuzidiwa na maradhi.
Alisema: “Kwangu mimi kufa ni kufa ila watu tunaogopa kutangulia. Sijui Diana alimaanisha nini ila nahisi alizidiwa. Unajua mtu akiwa anaumwa anaweza kusema neno lolote bila kukusudia, isitoshe hakunitaja peke yangu.”

Choki alipozungumza na gazeti hili alisema kwamba yeye katika maisha yake hakuwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Diana, hivyo haelewi ni kwanini alitajwa.
“Mimi nilikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Lillian Internet ambaye alikuwa rafiki yake, kuna watu ambao mimi nawajua ambao ndiyo hasa wanapaswa kuzungumziwa,” alisema Choki huku akiwataja wasanii wawili maarufu lakini wanahifadhiwa na gazeti hili.

Kwa upande wa Baba Diana, alisema kuwa yeye hajui chochote zaidi ya kuwa kiongozi wake kwenye bendi.
Alisema: “Sikuwahi kupita naye, najua Mr. Nice na Steve Nyerere waliwahi kuwa wapenzi wake na marafiki zake wakubwa ni Lillian Internet na Aisha Madinda.”

Banza Stone a.k.a Mwalimu wa Walimu alidai kwamba hajui chochote kuhusu tafsiri ya kile kilichozungumzwa na Diana, lakini akaeleza kuwa kuhusu kifo yeye hana shida kwa sababu anajitambua kama marehemu mtarajiwa.
“Mimi ni marehemu mtarajiwa, wakati wowote Mungu akinihitaji hata sasa, siwezi kumpinga, zaidi naweza sema labda alitoa kauli hiyo wakati hali yake ikiwa mbaya,” alisema Banza.

Katika ‘intavyuu’ na gazeti hili Machi 2009, Diana alitabiri kifo chake kwa kusema kuwa ugonjwa uliokuwa unamsumbua ulikuwa umekwishammaliza na kwamba asingeweza kupona.
Kwa kusindikiza kauli yake, Diana alisema kuwa tangu alipoanza kuugua, watu wengi ambao walikuwa marafiki zake kabla, walimtenga hata kwenda kumjulia hali.
HABARI KWA HISANI YA GLOBALPUBLISHERZ

No comments:

Post a Comment