Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Wednesday, May 26, 2010

Tanesco yapata Mrithi wa Dk. Rashid


Kile kiti cha moto cha Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kilichokuwa wazi baada ya Dk. Idris Rashid kumaliza muda wake tangu Novemba mwaka jana, kimepata mrithi.

Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco imemteua Mhandisi, William Geofrey Mhando, kuchukua nafasi hiyo. Uteuzi huo unaanza rasmi Juni mosi mwaka huu.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Tanesco jana, ilisema kuwa kabla ya hapo uteuzi huo, Mhando alikuwa ni Meneja Mkuu Usambazaji Umeme na Masoko katika shirika hilo lenye dhima ya kuzalisha na kusambaza umeme nchini.

Tangu Novemba mwaka jana Dk. Rashid baada ya kumaliza muda wake wa mkataba alikabidhi ofisi pamoja na nyumba ya Tanesco aliyokuwa akikaa na nafasi hiyo ilikuwa ikikaimu, Stephen Mabada.

Mhando aliajiriwa na Tanesco Oktoba 1987 kama mhandisi wa umeme, kabla ya kupanda cheo kuwa Mhandisi katika laini za umeme.

Mwaka 1990 hadi 1992 aliteuliwa kuwa Meneja wa Tanesco mkoa wa Singida na baadaye mwaka huo hadi 1994 alihamishiwa katika mkoa wa Mbeya kuwa Meneja wa mkoa wa Mbeya.

Vilevile Injinia Mhando alipandishwa cheo mwaka 1995 kuwa Mkurugenzi wa kanda ya Kusini Magharibi hadi mwaka 1999.

Taarifa hiyo imesema kuwa Mhandisi Mhando ana shahada ya uzamili ya umeme aliyoipata Havana, Cuba mwaka 1987, vile vile ana elimu aliyoipata katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Mhando anachukua nafasi iliyoachwa na Dk. Rashid ambaye aliingia Tanesco akiwa anatokea sekta binafsi alikokuwa akifanya kazi baada ya kuwa gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakati wa utawala wa awamu ya pili na tatu mwanzoni.

No comments:

Post a Comment