Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Sunday, May 2, 2010

Matokeo kidato cha sita: wasichana watamba!!!


JUMLA ya watahiniwa 55,764 sawa na asilimia 88.86 ya watahiniwa waliofanya mtihani wa Kidato cha Sita mwaka huu, wamefaulu ambapo idadi ya wasichana waliofaulu ni kubwa ikilinganishwa na idadi ya wavulana.

Jumla ya wasichana 21,821 sawa na asilimia 90.39 ya wasichana waliofanya mtihani huo wamefaulu, wakati wavulana waliofaulu ni 33,943 sawa na asilimia 87.90 ya wavulana waliofanya mtihani huo.

Akitangaza matokeo hayo jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Joyce Ndalichako alisema idadi ya watahiniwa waliofaulu imeongezeka kwa 10,048 wakati asilimia ya ufaulu imepungua kwa asilimia 0.78 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2009 ambapo waliofaulu ni 45,716 sawa na asilimia 89.64.

Alisema watahiniwa wa shule waliofaulu ni 45,217 , sawa na asilimia 93.76 ya waliofanya mtihani na watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu ni 10,547 sawa na asilimia 74.57.

Mwaka 2009 watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu ni 9,244 sawa na asilimia 74.84 ya waliofaulu. Hivyo idadi ya waliofaulu imeongezeka kwa watahiniwa 1,300 ikilinganishwa na mwaka jana.

Ingawa wasichana wanawaburuza wavulana kwa idadi ya waliofaulu, kwa mujibu wa matokeo nafasi ya wanafunzi kumi bora kitaifa inashikiliwa na wavulana waliokuwa wanasoma shule za sekondari za wavulana ambapo Sekondari ya Mzumbe inang’ara kwa kutoa wanafunzi bora wanne kati ya 10.

Walioshika nafasi ya kwanza hadi ya kumi kitaifa na shule zao kwenye mabano ni Japhet John (Ilboru), Manyanda Chitimbo (Kibaha), Hassan Rajab (Minaki), Samuel Killewo (Feza Boys), Abdullah Tahel, Steven Elias na Paul Nolasco wote wa Mzumbe Sekondari, Alexander Marwa (Tabora Boys) Ephraim Swilla (Mzumbe) na Benedicto Nyato (Tabora Boys).

No comments:

Post a Comment