Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Saturday, May 15, 2010

mtoto anayedaiwa kutekwa moshi na kupelekwa uganda alakiwa kishujaa



Mtoto anayedaiwa kutekwa nyara mjini moshi na kupelekwa nchini uganda akiwa amebebwa juu kwa juu muda mfupi baada ya kuwasili kwenye stendi ya basi ya kampuni ya Mabasi ya Kampala Coach Ijumaa hii.



Basi la Kampuni ya Kampala Couch lilipowasili jana mjini moshi kutokea Uganda ambalo lilikuwa na mtoto anayedaiwa kutekwa nyara watu wasio julikana na kupelekwa nchini Uganda .Hapa ni baadhi ya mamia ya watu waliojitokeza kumpokea mtoto huyo.



Pichani ni mtoto faraji Harun (8)anayedaiwa kutekwa nyara mjini moshi na kuepelekwa nchini uganda akiwa amebebwa juu kwa juu alipowasili Ijumaa
Picha zote na Habari na
Dixon Busagaga
wa Globu ya Jamii, Moshi

Mamia ya wakazi wa mji wa Moshi jana Ijumaa walikusanyika kumpokea mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili katika shule ya msingi ya Korongoni, mjini Moshi, alitekwa nyara Jumapili ya April 18, mwaka huu, muda wa saa 10 jioni, akiwa nyumbani kwao eneo la Oysterbay Mbuyuni, ambapo imedaiwa alisafirishwa kwa lori hadi nchini Uganda.

Baba wa mtoto huyo Haruni Ayoub (35), ambaye ni mfanyabiashara wa mjini Moshi, alisema kuwa mtoto wake huyo alitekwa nyara na watu hao wakati yeye na mama mzazi wa mtoto huyo Bi Bisina Abedi (32) wakiwa wamekwenda shamba.

Alisema alilazimika kwenda nchini Uganda kumwokoa mtoto wake, ambapo alisema wamefanikiwa kumwokoa baada ya kutimiza masharti yaliyotolewa na watekaji.

Imedaiwa kwamba watekaji hao, walifanya mawasiliano na wazazi wa mtoto huyo, na kumtaka kutoa fedha kiasi cha dola 1,000, ili waweze kumwachia mtoto huyo, lakini haijafahamika njia wazotumia kupata mawasiliano hayo.

Kwa mujibu wake Haruna walilazimika kutoa taarifa za tukio hilo katika kituo cha polisi mjini Moshi, lakini baadaye walilazimika kuandaa mchakato wa kutafuta fedha hizo, kutokana na vitisho na masharti magumu waliyoendelea kutolewa na watekaji hao, kwamba wameshampata mteja wa kumnunua mtoto huyo na wakichelewa hawataweza kumpata tena.

Kutokana na suala hilo kuelezewa kuwa gumu wazazi hao, kwa ushirikiano na wafanyabiashara wa soko la Mbuyuni, mjini Moshi, walichanga kiasi cha shilingi milioni 1.5, na kulazimika kusafiri hadi nchini Uganda wakifuata maelekezo ya watekaji hao, kwani waliambiwa mteja alishatoa shilingi milioni mbili ili kuweza kumnunua mtoto huyo

“Nilielekezwa kuweka fedha hizo kwenye akaunti katika benki ya Stanbic iliyopo eneo la Busia nchini Uganda kwenye akaunti namba 0140592455501 yenye jina la Salai Kaya na baadae tulisubiri kwa saa tisa, ambapo tulielekezwa kumchukua katika kituo cha mabasi cha Busia”, alisema.

Mtoto huyo, ambaye aliwasili mjini Moshi jana muda wa saa 6: 20 mchana, akiwa kwenye basi la kampuni ya Kampala Coach, lenye namba za usajili KBJ 989E, alimsha hisia za wafanyabiashara na wananchi wengine ambao walilitupia lawama jeshi la polisi kwa kushindwa kutoa ushirikiano wa kumpata mtoto huyo na kuwakamata watekaji.

Mara baada ya kupokelewa mtoto huyo huku akisindikizwa na umati mkubwa wa watu, alizungushwa katika maeneo mbali mbali ya mji wa Moshi, na baadaye kufikishwa nyumbani kwao, kwa ajili ya mapumziko.

Hata hivyo juhudi za askari kanzu waliofika nyumbani hapo kutaka mtoto huyo, kufikishwa katika kituo cha polisi ili kutoa maelezo, zilikutana na upinzani mkubwa wa wananchi, waliokuwa wakihoji kuwa walikuwa wapi hadi mtoto huyo anapatikana.

Akizungumza kwa taabu huku akibubujikwa na machozi ya furaha kwenye mahojiano na waandishi wa habari mtoto Faraji, alisema kuwa alipelekwa katika eneo asilolijua baada ya kuchukuliwa nyumbani kwao kwa ahadi ya kununuliwa mhindi wa kuchoma. Alisema amewaacha wenzake watatu, nchini Uganda , ambapo walikuwa wakiishi pamoja kwa muda wote huo.
Kwa upande wake Mkuu wa Upelelezi wa makosa ya jinai mkoani Kilimanjaro Bw. Linus Sinzumwa alithibitisha kupokea taarifa za kutekwa mtoto huyo na kueleza kuwa walikuwa wanaendesha uchunguzi wa kina kwa kushirikiana na askari wa mtandao wa kimataifa wa Interpol, kuwabaini watekaji hao.

Afande Sinzumwa, aliwaambia waandishi wa habari kuwa baba wa mtoto Haruna Ayoub, alitoa taarifa ya kupotelewa mtoto wake Mei 4, mwaka huu, baada ya kugundua amepotea tangu Aprili 18, mwaka huu.

Alisema jeshi hilo la polisi lilikuwa kwenye harakati za kutaka kuwasiliana na Interpol, ili kufanyia uchunguzi suala hilo , lakini baadaye mtoto huyo amepatikana wakati juhudi hizo zikiendelea, na kwamba bado juhudi zaidi za kuwasiliana na Interpol zinaendelea ili kuweza kubaini namba za simu zilizotumiwa na watekaji hao.

No comments:

Post a Comment