Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Friday, May 7, 2010

Mbunge na RC nusura wazichape hadharani!


Mbunge wa Simanjiro, Christopher Sendeka na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Henry Shekifu wameshutumiana na kushambuliana kwa maneno hadharani katika mkutano uliofanyika wiki iliyopita na mtiti huo kuonyeshwa jana na kituo kimoja cha televisheni.

Katika utetezi juu ya ugomvi wao uliotokea wakati wa mkutano uliohusisha viongozi wa serikali za vijiji vya Sukuro na Kitiangare, kila mmoja alimrushia mwenzake shutuma za kudhalilishana mbele za watu.

Kwa mujibu wa Ole Sendeka,anadai kuwa Mkuu wa Mkoa, ana ajenda ya siri dhidi yake, kwani tukio hilo lililotokea Ijumaa iliyopita si la kwanza la kumdhalilisha mbele ya wapiga kura wake.

Lakini Shekifu akijibu madai hayo, alidai kwamba Mbunge huyo amepungukiwa busara, kwani amekuwa na tabia ya kuvuruga vikao na akaonya kuwa ipo siku atamweka rumande ili kukomesha vitendo hivyo alivyodai ni vya utovu wa nidhamu.

Sendeka akitoa ufafanuzi katika sakata lake la kukwaruzana hadharani na Mkuu wa Mkoa, alidai chanzo cha mtafaruku ni mgogoro wa ardhi katika kijiji cha Sukuro wilayani humo.

Hata hivyo, Mbunge huyo alidai kuwa tofauti kati yake na Mkuu wa Mkoa ni za muda mrefu na mwaka juzi walikwaruzana hadharani katika kikao cha Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Manyara.

“Shekifu kama Mkuu wa Mkoa, amekuwa akijaribu kunidhalilisha mbele ya wananchi wangu na watu wengine… ni wazi kuwa ana ajenda yake binafsi dhidi yangu na mimi kwa sasa natafakari hatua za kuchukua dhidi yake,” alisema.

Mbunge huyo alidai kuwa wakati mkutano huo unaanza Mkuu wa Mkoa aliwataka viongozi wa vijiji na wajumbe wa serikali za vijiji kutoa maoni juuya kugawanywa kwa kijiji hicho na kumega eneo la ekari 45,000 kwa ajili ya mradi wa uwekezaji wa ranchi kwa shirika la Ilramatak.

“Baada ya wajumbe kuanza kutoa maoni yao, Shekifu alikataa ya wajumbe waliokuwa wanapinga mradi huo na kuamuru mjumbe aliyekuwa akitoa maoni yake akamatwe na Polisi kwa madai kuwa alivuruga mkutano huo,” alidai.

“Kutokana na kauli ya Mkuu wa Mkoa mimi Mbunge niliingilia kati na kuwaambia polisi wasimkamate mjumbe huyo, kwa sababu hakuwa na kosa lolote… hapo ndipo RC alipokuja juu na kuwataka polisi wanikamate,” alidai.

Aliendelea kudai kuwa wananchi wa vijiji vitano vya Terrat, Nadonjukin, Sukuro, Kitiangare na Naberera, wamekuwa na mgogoro wa muda mrefu na Ilramatak shirika ambalo linataka kuwekeza mradi huo katika eneo la wazi linalokutanisha vijiji hivyo, ambalo linatumika kama mbuga ya malisho kwa wafugaji.

Alidai kuwa wananchi wamekuwa wakipinga mradi huo, kutokana na kwamba eneo hilo wamekuwa wakilitumia kwa ufugaji kwa miaka mingi na pia hutumika kama mapito na malisho ya wanyamapori wanaotoka hifadhi ya Taifa Tarangire.

Mbunge alidai kuwa kilichomshangaza katika mkutano huo ni hatua ya kuruhusiwa kwa viongozi wa shirika linalotuhumiwa na wananchi kuwa linataka kupora ardhi yao, kushiriki mkutano wa viongozi wa vijiji na Mkuu wa Mkoa, huku wakiwa wamekaa meza kuu.

Mbunge huyo alisema hata hivyo baadaye walimaliza tofauti hizo na kuendelea na mkutano huo ambao hata hivyo uliahirishwa baada ya tafrani hiyo.

Shekifu alikanusha madai ya kumdhalilisha Mbunge huyo ila akamtupia lawama Sendeka kuwa ndiye amekuwa na tabia za kudhalilisha Serikali mbele ya wananchi.

Mkuu wa Mkoa alidai kuwa chanzo cha mtafaruku wa juzi ni kugawanywa kwa vitongoji wala si ardhi kama anavyodai Mbunge huyo. Hata hivyo, Shekifu alidai amesamehe yote yalifanywa na Mbunge huyo wa Simanjiro.

Alidai kwamba kitendo cha Sendeka kumkataza Mkuu wa Polisi wa Wilaya kumtoa mwananchi ambaye alikuwa anafanya fujo kwenye kikao hicho, kinaonesha jinsi Mbunge huyo asivyoiheshimu Serikali.

Hivi karibuni, Sendeka alifutiwa kesi dhidi yake iliyokuwa ikidai kuwa alimpiga na kumtishia bastola Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM wa Mkoa wa Arusha, James ole Milya.

No comments:

Post a Comment