Psquare Ft. J.Martins- E No Easy

Thursday, May 27, 2010

Maimamu wamkana dogo aliyetaka kulipua UBALOZI!


Shura ya Maimamu Tanzania, imekanusha taarifa kwamba yule dogo anayetuhumiwa kwa jaribio la ulipuaji wa Ubalozi wa Marekani nchini, alihamasishwa na mawaidha ya shehe wa msikiti wa Mtambani.

Aidha, imesema taarifa hiyo ilikuzwa kwa lengo la kuipaka matope shule ya msingi Mtambani ambayo mwaka jana ilitoa mwanafunzi bora wa somo la Sayansi katika mtihani wa Taifa wa darasa la saba.

Katibu Mkuu wa Shura hiyo, Shehe Ponda Issa Ponda, alisema jana kwamba shule hiyo haina rekodi inayoonesha kwamba mtuhumiwa huyo, mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Biafra, Nassib Mpamka (15) aliwahi kufika hapo.

“Tukio hilo limepangwa kuharibu sifa nzuri ya shule ya Mtambani, kwani imepata mafanikio ya kitaaluma,” alisema.

Alipotakiwa kuzungumzia jaribio la kulipua Ubalozi wa Marekani, alikataa kuzungumzia chochote akidai kuwa suala hilo halijatolewa uamuzi na mahakama.

“Waislamu ni watu wazuri na wanapenda amani, lakini maadui zetu wanawafanya waonekane magaidi ili kutimiza malengo yao mabaya,” alisema.

Alisema Shura ya Maimamu imepanga kuandamana ili kusafisha picha mbaya iliyoenea kuwa walimu wa shule ya msingi Mtambani wanahusika na jaribio la kulipua Ubalozi wa Marekani.

“Inawezekana tukio hili limetungwa, ili kuwafanya Waislamu wasiuangalie Uchaguzi Mkuu ujao,” alisema.

Mei 16 mwaka huu saa 2.30 usiku, inadaiwa Nassib alifika katika ubalozi huo eneo la kuegesha magari na kurusha chupa iliyokuwa na mafuta ya taa na utambi kwa lengo la kulipua magari hayo.

Mwanafunzi huyo baada ya kuhojiwa na Polisi, alidai kuwa alihamasishwa na mahubiri ya shehe wa Msikiti wa Mtambani kuhusu majeshi ya Marekani kuua Waislamu duniani.

No comments:

Post a Comment